Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
imesema, mpaka sasa haijafahamika kinachosababisha ugonjwa wa Lupa, ambao umeua mtu mmoja huku 10 wakiwa wanafuatiliwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile,
jana Septemba 06, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 03 mkutano
wa 12 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu
swali la la Mbunge, Asha Jecha, aliyetaka kufahamu chanzo cha ugonjwa
wa Lupa pamoja na idadi ya watu walioguwa na kufariki nchini.
"Hadi
sasa watafiti hawajaweza kujua chanzo cha ugonjwa wa Lupa, inasadikiwa
mgonjwa mwenye vinasaba vya Lupa, hupata ugonjwa huo pale anapopatwa na
visababishi kwenye mazingira yanayochochea kupata maradhi hayo. Vitu
vinavyochangia kupata ugonjwa huo ni miale ya jua, maambukizi ya
bakteria, matumizi baadhi ya dawa ya shinikizo la damu, dawa za kifafa
na 'antibiotic", alisema Dkt. Ndugulile na kuongeza;
"Ugonjwa
wa Lupa ni ugonjwa wa kinga za mwili ambao hushambulia viungo vya mwili
vikidhania kwamba ni vitu vigeni. Viungo ambavyo hudhurika zaidi ni
ngozi, figo, ubongo, chembe chembe za damu, moyo, mapafu na viungo
vingine vya mwili kama 'joint".
Aidha,
Dkt. Ndugulile alisema ugonjwa huo huwapata zaidi watu wenye jinsia ya
kike (wanawake) wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi kufikia 45.
"Ugonjwa
huu hauna tiba bali hutolewa dawa za kupunguza athari tu, katika
hospitali ya Muhimbili hugundulika watu wenye ugonjwa huu wawili kwa
kila mwaka na hupatiwa tiba kwenye kliniki ya ngozi, na hadi hivi sasa
kuna wagonjwa takribani 10 wanaofuatiliwa", alisisitiza Dkt. Faustine.
Kwa
upande mwingine, serikali imesema imejipanga kutekeleza mikakati
mbalimbali ikiwamo kutekeleza mkakati wa nne wa taifa wa kudhibiti
UKIMWI wa mwaka 2018 hadi 2023, ili kumaliza au kutokomeza kabisa
ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoadhimiwa na Umoja wa Mataifa.
Mpekuzi.
Comments