Serikali
imetumia kiasi cha shilingi bilioni 216 kukamilisha mradi wa Umeme wa
Makambako hadi Songea ikiwa ni moja ya miradi ya kimkakati yenye lengo
ya kufanikisha sera ya Tanzania ya viwanda.
Akizungumza
katika kipindi cha TUNATEKELEZA, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani
amesema kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Septemba mitambo ya mradi huo
itawashwa na wananchi wa mikoa ya Njombe na Ruvuma wataanza kufurahia
umeme wa uhakika kutoka gridi ya taifa.
“Mradi
huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani wataunganishiwa umeme
kwa bei nafuu ya mradi wa REA ambayo ni elfu 27 tu na kuwanufaisha
wateja 22,700 hali itakayowawezesha wananchi kutumia umeme huo kwa
ujenzi wa viwanda na shughuli za maendeleo katika maeneo yao”
Alisisitiza Dkt. Kalemani
Akifafanua
zaidi Dkt. Kalemani amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaokoa
fedha kiasi cha Shilingi bilioni 9.1 ambazo zinatumika kununua mafuta
mazito yanayotumika kwenye mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Madaba,
Ludewa, Mbinga, Namtumbo na Songea Mjini.
Akielezea
ujenzi wa mradi huo uliotekelezwa na Serikali ya Tanznaia kwa
kuhsirikiana na Serikali ya Sweden, Waziri Kalemani amesema mradi huo
umetekelezwa kwa awamu mbili. “Sehemu ya kwanza ya mradi huu
imehusisha ujenzi wa vituo vitatu vya kupooza na kusambaza umeme mkubwa
wa msongo wa KV 220 vilivyojengwa Makambako, Madaba na Songea na sehemu
ya pili ilihusisha ujenzi wa miundo mbinu ya kusafirisha umeme”.
Akizungumzia
mradi wa REA awamu ya tatu ambao unatarajiwa kuunganisha vijiji 5100
kwenye mtandao wa umeme Dkt. Kalemani amesema vijiji 818 tayari
vimeshaunganishwa tokea kuanza kwa mradi huo mwezi Julai mwaka huu.
Aliongeza
kuwa lengo la Serikali kufikisha umeme katika Vijiji 12,268 ni
kutekeleza azma ya kufikisha umeme kwa kila mwananchi bila kujali
anaishi mjini au kijijini ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Kwa
upande wa mradi wa Kinyerezi Dkt. Kalemani amesema mradi huo
umekamilika kwa asilimia 100 na megawati 218 tayari zimeshaingizwa
kwenye gridi ya Taifa. Megawati za umeme zilizobaki zinatarajiwa
kuingizwa kwenye gridi ya taifa kabla ya mwanzo wa mwezi Oktoba.
Mpekuzi.
Comments