Agizo la Rais Magufuli Laanza Kutekelezwa....Nemc, Mkemia Mkuu wa Serikali wachukua sampuli maji yenye Sumu.
Wataalamu
kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wamechukua sampuli zaidi ya kumi ya
maji kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi,
ili kuona kama maji hayo yana kemikali zenye madhara kwa viumbe hai.
Sampuli
ya maji hayo yanayodhaniwa kuwa na kemikali yanayotiririka kutoka
katika mgodi wa Acacia North Mara mpaka kwenye makazi ya watu.
Uchukuaji wa sampuli hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni alipokuwa ziarani mkoani Mara.
Akizungumza
wakati zoezi hilo likiendelea, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk.
Vedast Makota, alisema kuwa NEMC imeanza kutekeleza agizo hilo kwa
kuchukua sampuli katika maeneo yote ili kubaini kama zina madhara kwa
viumbe hai au la.
“
NEMC kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali watafika kila
mahala ikiwamo kupitia vibali vyote vya awali ili kubaini kama
utolewaji wa vibali hivyo ulikidhi vigezo vinavyotakiwa na kuona kama
wamiliki wa mgodi huo wanazingatia masharti yaliyoagizwa katika vibali
hivyo,” Dk. Makota alisisitiza.
Alisema
utafiti wao utaenda sambamba na uchukuaji sampuli mbalimbali yakiwamo
maji, mimea na mchanga ambapo watahakikisha wanashirikiana na jamii
inayozunguka mgodi huo ili kufanikisha zoezi zima kuona kama kuna
viashiria vinavyoshukiwa kuwa na chembe chembe zenye kemikali.
“Tupo
katika hatua za awali za utekelezaji wa agizo hilo ambapo wataalamu
wametembelea maeneo ya Mto Tigite, ambao kwa kiasi kikubwa maji yake
ndiyo yanatumika sana kwa wakazi wa eneo hilo katika shughuli mbalimbali
za kijamii,” alisema.
Alisema
wameshatembelea mabwawa mbalimbali yanayotumika kuhifadhia tope sumu
(TFS) zinazotokana na shughuli za mgodi huo, ikiwamo wataalamu kutoka
kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua sampuli mbalimbali ambazo
zitapelekwa maabara kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu.
“Baada
ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchukuaji sampuli hizo na kubaini
ukiukwaji wa sheria za mazingira ni wazi kuwa NEMC haitosita kuchukua
hatua kali za kisheria kwa mmiliki ili iwe fundisho kwa wengine,”
alisema.
Naye
Meneja wa Kanda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Venkya Masambu,
alisema kwa kutambua uharibifu mkubwa unajitokeza katika maeneo ya
migodini, ofisi yake kwa kushirikiana na NEMC waliamua kuchukua sampuli
hizo upya ambazo watazipeleka katika maabara ya serikali yenye wataalamu
waliobobea.
“Endapo
sampuli zitakazopelekwa kwa Mkemia Mkuu zitabainika kuwa na madhara kwa
binadamu hawatasita kutoa ushauri kwa wamiliki wa mgodi, ili kuona
namna gani ya kutatua dosari zinazoweza kujitokeza,” alisema.
Mratibu
wa Uendeshaji Idara ya Uchenjuaji Dhahabu wa Acacia North Mara, Patice
Kabazimu, alisema wamewapokea wataalamu hao na watahakikisha wanawapatia
ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi yao.
“Sisi
kama Acacia tunatambua umuhimu wa zoezi linalofanywa na wataalamu hawa
ili kuleta ustawi na maendeleo kwa jamii yetu,” alisema.
Mpekuzi.
Comments