WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini washirikiane na
Madiwani katika halmashauri zao wafanye tathmini ya mali zote
zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili
kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya
uchumi kwa sasa.
Amesema
licha ya tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia
itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza
wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kiduchu, jambo
linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza
na watumishi wa halmashauri ya Mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya
ya Nzega pamoja na Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa
Nzega akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Nzega, Tabora.
Ametoa
agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba Serikali
iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara
kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega
ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa
makubaliano ya kulipa kodi.
Uongozi
wa halmashauri ya Mji wa Nzega uliamua kupitia upya mkataba wa mradi
huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi, hivyo ilianzisha mpango wa
maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati waliokuwa wakiwatoza
wafanyabiashara zaidi ya sh 150,000 kwa mwenzi na kuilipa halmashauri
sh. 30,000 kwa mwezi.
Pia
ilibaini kwamba baadhi ya wamiliki wa awali wa vibanda waliviuza kwa
wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya kuishirikisha halmashauri
na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara waendelee kuwa wapangaji
kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka mgogoro wa umiliki wa
vibanda hivyo.
Waziri
Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo huwa haiishi kwa wakati katika
maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo vinamilikiwa na Wakuu wa
Idara, Madiwani na baadhi ya watumishi katika hailashauri husika, jambo
linalozikosesha halmashauri mapato. “Wakuu wa wilaya shughulikieni
hili,”.
Pia,
Waziri Mkuu amezishauri halmashauri zinazomiliki vibanda vya biashara
hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie leseni za biasahara
zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na wamiliki wake ili
kuondoa uwepo wa mtu wa kati.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wanaomiliki vinanda vya
biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za umiliki wao ili kuondoa
mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya kujadili namna
bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara
vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri na wilaya
wawahamasishe wananchi kwenye maeneo yao juu ya umuhimu wa kujiunga na
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), hivyo watakuwa wamejihakikishia
upatikanaji wa huduma za afya bure kwao na familia zao.
Pia
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Agrey Mwanri kwa jitihada kubwa
za kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya kupitia CHF, ambapo kwa
mkoa huo wanachama wa mfuko huo wanaweza kutibiwa kwenye hospitali zote
za Serikali tofauti na maeneo mengine ambayo huduma hiyo inaishia kwenye
hospitali za wilaya tu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.
Mpekuzi.
Comments