Rais
Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum
kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini
Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.
Hii
inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo
awali alimtembelea Agosti 8,2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela
akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15,2018 katika wodi ya
Taasisi ya Mifupa MOI.
Akiwa
hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na
kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu aendelee na
majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya
katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za
Maliasili.
“Nikutakie
kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa
upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza
kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza
Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.
Tayari
jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa
sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea
nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto
ambao kila siku unaendelea kuimarika.
Hata
hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake
inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea
nyumbani huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.
Aidha,
jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea
umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali
hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa
kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa
ya sita.
Waziri
Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko
Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa
na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku
watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini
hapo.
Mpekuzi.
Comments