Na John Mapepele
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua mikakati 15 itakayotumika
kama nyenzo ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo na
kuleta mageuzi makubwa na ya muda mfupi kwenye sekta za mifugo na uvuvi
kabla ya kumalizika awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya awamu ya
tano mwaka 2020.
Mikakati
hiyo ni pamoja nakudhibiti magonjwa ya mifugo chanjo na viatilifu,
mpango kazi wa kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya
mifugo na mazao yake, mkakati wa usimamizi na udhibiti wa rasilimali za
uvuvi nchini, mkakati wa upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji kwa
ajili ya mifugo pamoja na mkakati wa kuboresha na kuzalisha kwa wingi
ng’ombe wa nyama na maziwa kwa njia ya uhimilishaji.
Mwingine
ni mkakati wa kudhibiti na kuondoa migogoro baina ya wakulima, wafugaji
na watumiaji wengine wa ardhi, mkakati wa kuboresha uzalishaji wa
kuku,mkakati wa kuanzisha na kuwezesha ushirika wa wafugaji, mkakati wa
kuendeleza ukuzaji wa viumbe kwenye maji pamoja mkakati wa kufufua
Shirika la Uvuvi nchini TAFICO
Akizungumza
jijini Dodoma mara baada ya kuzindua mikakati hiyo, Waziri Mpina
ameiagiza wizara hiyo kuunda kikosi kazi kitakachosimamia utekelezaji
wake na kwamba kila baada ya miezi mitatu kufanyike tathmini na kwa
watumishi wataoshindwa au kukwamisha utekelezaji wa mikakati hiyo
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na taratibu.
Alisema
mikakati hiyo ikikamilika Serikali itaweza kukusanya zaidi ya sh
bilioni 100 kwa mwaka zitokanazo na sekta za mifugo na uvuvi tofauti na
sh bilioni 30 zilizokusanywa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 ambapo
kwa mwaka 2017/2018 Serikali imeweza kukusanya sh bilioni 46 baada
kufanyika Operesheni Sangara na Nzagamba.
Hivyo
Waziri Mpina alisisitiza kuwa utoroshaji wa mazao ya mifugo nje ya
nchi, uvuvi haramu,mifugo kufa kwa kukosa tiba sahihi za magonjwa kwa
wakati havitapata tena nafasi chini ya uongozi wake huku ulinzi wa
rasilimali za mifugo na uvuvi ukiimarishwa kwa kuweka vizuizi katika
njia zote zilizobainika kuhusika na utoroshwaji huo.
Alisema
udhibiti wa magonjwa ya mifugo utawezesha kuongeza uzalishaji kuanzia
ndege wafugwao, mbuzi, kondoo,ng’ombe na kuchochea uwekezaji katika
viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo hapa nchini na kuwezesha
upatikanaji wa ajira,kodi na upatikanaji wa bidhaa za mifugo kwa gharama
nafuu.
Waziri
Mpina alisema ni aibu kwa Taifa ambalo asilimia 37 ya nchi yake ni maji
na yenye uoto wa asili mzuri lakini tunashuhudia mifugo ikidhoofika na
mingine hata kufa kwa kukosa maji na malisho hivyo mkakati huo utatoa
majawabu ya changamoto hiyo.
Pia
alishangazwa na kitendo cha baadhi ya watu wakihodhi mashamba ya mifugo
ya Serikali waliobinafsishiwa na kubadilishiwa matumizi na kwamba kwa
miaka mingi wameshindwa kuendeleza mashamba hayo hivyo Serikali
itayataifisha yote na kurejeshwa serikalini ili yatumike kulishia
mifugo.
Pia
mikakati hiyo itamaliza kabisa tatizo la wafugaji kukosa haki ya kupata
malisho kutokana na migogoro ya ardhi huku akitolea mfano mnada wa Pugu
wenye ukubwa wa ekari 1,900 lakini sasa zimebaki ekari 108 tu baada ya
wananchi wengi kuvamia eneo la mnada na kugeuza makazi.
Waziri
Mpina alisema mikakati hiyo ndio itakuwa mwarobaini wa matatizo yote
yaliyokuwa yanakabili sekta ya mifugo na uvuvi , na kuziagiza
halmashauri zote nchini nazo zishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa
mikakati ili kuiwezesha sekta ya mifugo na uvuvi kutoa mchango
unaostahili katika pato la taifa.
Hivyo
Wizara itaandaa mafunzo kwa maofisa Mifugo na Uvuvi kutoka katika
halmashauri zote nchini mwezi Agosti ili kuwawezesha kuufahamu mkakati
huo na kuutekeleza kwa umakini na kwa wakati.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mkuu-Mifugo, Celina Lyimo alisema kuandaliwa
kwa mikakati hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mpina alilolitoa
Julai 6 mwaka huu la kutaka kuandaliwa mikakati ya kuwezesha kuwepo
mageuzi katika sekta hizo na kuwataka watumishi wa wizara hiyo kuifanyia
kazi kwa wakati weledi na uadilifu ili kupata matokeo chanya katika
kipindi kifupi.
Naye
Kaimu Katibu Mkuu-Uvuvi, Julius Mairi alisema mikakati hiyo itawezesha
sekta za mifugo na uvuvi kuwezesha kuongeza pato la Taifa na mtu mmoja
mmoja na kumshukuru Waziri Mpina kwa uongozi wake thabiti uliolenga
kuona kunakuwepo mageuzi ya haraka kwenye sekta hizo.
Mpekuzi.
Comments