Moto wateketeza maduka Melitano.

MOTO mkubwa umezuka na kusababisha kuungua kwa maduka mawili huko Melitano Msikitini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kusababisha hasara kubwa.
Taarifa hiyo, imetolewa na Mkuu wa kituo cha Zimamoto Mjini, Suleiman Ahmada wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake Kilimani.
Alisema, chanzo cha moto huo inasadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme ambayo ilianzia katika duka la chakula na kuendelea katika duka la vinywaji na kuunguza vitu mbalimbali.
Mkuu huyo alisema mmliki wa maduka hayo ni Abdallah Rashid Ali (45) mkaazi wa Melitano na kueleza kuwa mmliki huyo aliweza kuona moshi mkubwa ukitokea ndani ya duka la chakula ambalo ndani yake kulikua na friji.
Alisema, hasara iliyopatikana katika ajali hiyo ni kubwa hivyo, amewataka wananchi kuzikatia bima mali zao ikiwemo nyumba na maduka ili kuondokana na unyonge unaoweza kujitokeza baada ya kukubwa na majanga mbalimbali.
Aidha alifahamisha kuwa hivi sasa kumekuwa na ongezeko la matukio ya ajali za moto sehemu mbalimbali na kubainika kuwa nyumba na maduka mengi hazijakatiwa bima.
Alisema, kufanya hivyo kutaweza kusaidia kurejeshewa gharama za mali zao, lakini kwenda kinyume na hilo kutasababisha kuingia katika unyonge wa kudumu kwa sababu suala la moto likija halitoi taarifa.
Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Gesawda Sedoyeka aliwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa katika masuala ya umeme kwa kuhakikisha kuwa wanapotoka aidha katika nyumba au sehemu zao za kazi kuzima swichi.
Zanzibarleo.

Comments