Chadema
kimesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) inapaswa kulaumiwa kwa kuvuruga
uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, 2018, kuorodhesha baadhi ya
matukio iliyodai yalilenga kuwakandamiza wagombea wa chama hicho na
wanachama.
Jana
Alhamisi Agosti 16, 2018 chama hicho kilitoa taarifa kwa vyombo vya
habari na kubainisha kuwa baadhi ya maeneo wagombea wake walienguliwa
katika mazingira ya kutatanisha, hata walipojaribu kuhoji hakuna hatua
zozote zilizochukuliwa.
Chama
hicho kimesema taarifa iliyotolewa na NEC kujibu tamko la Ubalozi wa
Marekani kuhusu uchaguzi huo mdogo, haiakisi ukweli wa mambo na
badala yake ilipotosha kuhusu kilichotokea kwenye mchakato wa uchaguzi
huo.
Taarifa
hiyo iliyotolewa na ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene inasema
NEC imeshindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, kutokana na ama
kutokuwa na uwezo au kufumbia kwa makusudi hila na njama zilizokuwa
zikifanyika kuharibu na kuvuruga uchaguzi huo.
“Jamii
ya watanzania, jumuiya ya kimataifa na dunia nzima iliona na kushuhudia
kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo vyombo vya habari
na mitandao ya kijamii jinsi ambavyo NEC ilishindwa kusimamia uchaguzi
uwe huru na haki,” ilisema.
“Mathalani
wagombea udiwani wa Chadema katika kata tano Tunduma walinyimwa fomu
zao za kugombea kwa makusudi kabisa kisha fomu hizo wakapewa watu
wengine (wanaodaiwa hawajulikani).”
Imesema,
“kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha kughushi. Kama hiyo
haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na polisi na
kubambikiwa tuhuma za jinai.”
Mbali
na hoja hizo, Chadema imesema imeshangazwa na namna NEC ilivyohoji
Marekani ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa uchaguzi
uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
“Swali
hilo la NEC linaibua swali jingine, je mamlaka zilizoharibu na
kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna
waangalizi wa kimataifa? Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za
matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya,” imesema
taarifa hiyo.
Agosti
15, 2018 NEC iliutaka ubalozi huo kuthibitisha inachokieleza juu ya
uchaguzi huo, ikisema uchaguzi mdogo huwa hauna waangalizi wa kimataifa
na kuhoji ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo na hayo iliyoyaona ni kwa
kutumia utaratibu upi na sheria ipi.
Mpekuzi.
Comments