Gesi Asilia Iko Tayari Mtwara....Kwa Mwezi ni 25,000 tu Badala ya Kununua Mtungi wa Gesi kwa 55,000.
WAZIRI
wa Nishati, Dk Medard Kalemani amezindua mradi wa ujenzi wa mtambo wa
kusambaza gesi asilia majumbani mkoani Mtwara, ambao baada ya miezi
mitatu watumiaji 150 wataanza kunufaika.
Dk
Kalemani alizindua mradi huo juzi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi
ya Mtwara baada ya kuzindua megawati nne za umeme katika Kituo cha Umeme
cha Mtwara.
Alisema
ujenzi wa mtambo huu umegharimu jumla ya Sh billioni 1.5 kwa ajili ya
kuwapelekea watumiaji wa awali wasiopungua 150 ambao baada ya miezi
mitatu, wataanza kutumia gesi hiyo majumbani.
Aliongeza
kuwa matumizi ya gesi asilia ni madogo sana yaani ni kama hayapo, kwa
kuwa wananchi wengi wanatumia kuni na mkaa kuliko gesi.
“Sasa
mtungi wa gesi ni takriban Sh 55,000, lakini ukitumia gesi asilia kwa
matumizi ya nyumbani itakuwa Sh 25,000 na utatumia kwa mwezi mzima hivyo
ni nafuu kwa mwananchi wa Tanzania,” alisema.
“Mwezi
Mei tulianza matumizi ya gesi majumbani, lakini leo tumeanza matumizi
ya gesi asilia katika Mkoa wa Mtwara. Hayawi hayawi yamekuwa,” alisema.
Aidha,
alieleza kuwa kuna magari zaidi ya 100 yanatumia gesi asilia jijini Dar
es Salaam, hivyo kuazia Machi mwakani, wataanza usanifu ili magari ya
Mkoa wa Mtwara nayo yaanze kutumia gesi asilia.
Alitoa
mwito kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuanza kutoa
elimu mara moja kwa wiki kwa Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara ili
kuhakikisha kuwa wanafunzi na walimu wa shule hiyo wanapata uelewa mzuri
katika matumizi ya gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani.
Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alieleza kuwa “umeme tunaoutumia
kwa sasa, asilimia 60 inatokana na gesi asilia na sasa gesi hii inaweza
kutumika kwa matumizi ya majumbani na wananchi watanufaika moja kwa moja
na gesi asilia inayozalishwa kutoka Mkoa wa Mtwara”.
Naye
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia alimpongeza Dk Kalemani kwa kuwa
msikivu na mwepesi wa kutimiza ahadi zake kwa wabunge wenzake.
Alitoa
mwito kwa TPDC kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wa Mtwara na
Lindi ili kuondoa woga na kuwaelimisha matumizi bora ya gesi asilia.
Mpekuzi.
Comments