Bilioni 11 Zatengwa Kuwanufaisha Vijana Wajikwamue Kimaisha.

Vijana 30,000 kutoka Mikoa ya Iringa, Mbeya na Mikoa ya Tanzania Visiwani watanufaika na fursa ya mafunzo ya kilimo na ujasiriamali kupitia Program ya Feed the Future inayofadhiliwa na Shirila la Misaada la Marekani (USAID) ambapo watapewa nyenzo na mtaji yenye thamani ya Sh. Bilioni 11.

Hayo yasememwa jana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana na Ajira, Anthony  Mavunde akiwa mkoani Iringa wakati akizindua Baraza la Vijana la Ushauri wa Mradi.

Mavunde alisema katika mradi huo vijana watapewa nyenzo na mitaji ya kuanzia shughuli za uzalishaji mali, ambapo amelitaka Baraza hilo kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa hasa katika kumkomboa kijana wa kitanzania na changamoto za ukosefu wa ajira na kumsaidia kufikia malengo yake.

Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk.Inmi Patterson alisema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza ujuzi wa Nguvu kazi ya Vijana wa Tanzania na kuhamasisha ushiriki wao katika sekta ya kilimo ili kuongeza pato la Taifa zaidi kupitia sekta ya Kilimo ambayo imeajiri Watanzania wengi.

Kwa upande wa  Kaimu Mkuu Mkoa wa Iringa, Richard Kasesela ameahidi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ambao utawanufaisha Vijana wa Iringa kwa kiasi kikubwa.
Mpekuzi.

Comments