Wabunge Wa Kigoma Waridhishwa Na Utendaji Wa Serikali ......Waipongeza kwa kampeni ya kuhamasisha kilimo cha michikichi.
WABUNGE
wa mkoa wa Kigoma wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha kilimo
cha zao la michikichi kwa sababu litasaidia kuondoa umasiki kwa wananchi
wa mkoa huo.
Wamesema
kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba Serikali kulifufua zao hilo kwa kuwa
ndilo zao kubwa la biashara linalotegemewa na wananchi wengi wa mkoa
huo, hivyo kitendo cha kuanzisha kampeni hiyo kinaonesha dhamira ya
dhati ya Serikali ya kuwakwamua wananchi.
Wakizungumza
kwa jana (Jumamosi, Julai 28, 2018) wabunge hao waliahidi kushirikiana
na Serikali bega kwa bega kuhakikisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha
zao la michikichi linafanikiwa kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Wabunge
hao waliyasema hayo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua
kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi katika mkutano
uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma. Mkutano huo
ulihudhuriwa na wadau wa zao hilo.
Miongoni
mwa wabunge hao ni mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye
aliipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrfu cha wananchi wa
mkoa huo cha kufufuliwa kwa zao la michikichi kwa kuwa litakwenda
kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Kigoma.
“Nakupongeza
Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa kitendo hiki cha kufufua
zao la michikichi kwani hiki ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi wa
Kigoma kwa hatu hii naamini kuwa leo hata waliotangulia mbele ya haki
watakuwa wanatabasamu huko waliko,”.
Pia
mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi na viongozi wa
mkoa wa Kigoma kuwa ni vema wakashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha
zao hilo linafufuliwa kwa watu kuchangamkia fursa ya kupanda michikichi
kwenye mashamba yao.
Mbunge
mwingine wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba alisema
changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa mkoa huo ni upatikanaji wa
mbegu bora za michikichi, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia katika
upatikanaji wa mbegu.
Kwa
upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Trade Mark Bw. John Luaga alisema
walifanya utafiti kuhusu zao la michikichi na walibaini kuwa kuna soko
kubwa la mafuta ya mawese ndani ya nchi yetu, pamoja na nchi za jirani
ila uzalishaji wa mafuta hayo ndani ya nchi bado ni mdogo sana.
Alisema
hali inachangiwa na kuwepo kwavikwazo vichache vinavyokwamisha ongezeko
la uzalishaji wa ndani, ambavyo ni matumizi ya teknologia hafifu katika
kilimo cha mchikichi, na ukamuaji wa mafuta ya mawese.
Pia
ukosefu wa miundombinu na usafiri, ukosefu wa maghala ya kukusanyia
matunda ngazi ya wilaya, na badala yake mkulima mmoja mmoja anahangaika
kupeleka kwa mteja hivyo kumuongezea gharama, ukubwa wa gharama za
usafiri kutoka shambani mpaka sokoni.
Naye,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB), Bw. Josephat Faustine alisema kilimo cha zao la michikichi kina
faida kubwa na kinawekezeka, hivyo wao wataanisha maeneo yote yanayofaa
kuwekeza.
Pia
Mkurugenzi huyo wa TADB alisema benki yao inauwezo wa kutoa mikopo ya
mitaji kwa vituo vya uzalishaji mbegu za zao la michikichi na kumaliza
changamoto ya upatikanaji wa mbegu, hivyo ni muhimu kwa wakala wa mbegu
kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kufufua zao hilo
na kwamba changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la michikichi
ikiwemoya upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa ajili ya kununua mbegu au
miche mipya zinafanyiwa kazi.
Waziri
Mkuu alisema Serikali itahakikisha zao hilo linafufuliwa na kulimwa kwa
wingi mkoani Kigoma pamoja na mikoa mingine inayolima michikichi
nchini, ambapo amewata Maafisa Kilimo katika ngazi zote waanzishe
mashamba ya michikichi.
Pia
amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchi kuhakikisha mashamba ya
wananchi yanapimwa na wahusika kupewa hati ili ziwaweze kupata dhamana
ya mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha na kuwekeza kwenye
kilimo.
Waziri
Mkuu alisema halmashauri zinazolima michikichi viongozi wake wantakiwa
kuanzisha vitalu vya miche ya zao hilo na watakaoshindwa kuanzisha
vitalu hivyo pamoja na kuhamasisha kilimo cha michikichi kwenye maeneo
yao wajitathimini mwenyewe.
Aliongeza
kuwa kuanzia sasa mkoa huo uhakikishe miche ya michikichi inapandwa
katika maeneo yote yakiwemo ya pembezoni mwa barabara, katika mashamba
ya shule za msingi na sekondari, kambi ya JKT na kwenye magereza na
kwenye makazi ya wananchi.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alitoa angalizo kwa wawekezaji watakaowekeza katika
kilimo cha michikichi kutoanzisha migogoro na wananchi watakaowakuta
katika maeneo yao na badala yake washirikiane nao vizuri kwa sababu
migogoro haina tija kwao na kwa wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Mpekuzi.
Comments