Watu
wanne wakiwamo wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashtaka manane ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi saini ya Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba
katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliwataja washtakiwa hao jana
mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde kuwa ni Ofisa wa
Mazingira NEMC, Deusdith Bulamire (38), Sekretari, Edna Lutanjuka (51)
na mkulima Mwaruka Mwaruka (42).
Mwingine ni Mkaguzi kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), Dawson Barwongeza.
Akisoma
mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, wakili Katuga alidai washtakiwa
hao kwa pamoja kati ya Machi 28, 2017 na Novemba 4, 2017 wakiwa Dar es
Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi Vyeti vya Tathmini ya
Uharibifu wa Mazingira (EIA).
Washtakiwa
Bulamire, Lutanjuka na Mwarukwa wanadaiwa kuwa Oktoba 10, 2017
walighushi saini ya Waziri Makamba kwenye cheti cha EIA wakijaribu
kuonesha sahihi hiyo ni ya waziri huyo wakati si kweli.
Kwa
pamoja washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Machi 28 na Novemba
4, mwaka jana walijipatia Sh30 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka
kwa F1195 CPL Yohana Mtweve kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathmini ya
uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na NEMC
kitendo ambacho si kweli.
Pia, wanadaiwa kuisababishia hasara ya Sh20 milioni NEMC.
Baada
ya kusomewa mashtaka hayo hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu
Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza wala kutoa dhamana
kwenye kesi hiyo.
Washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi iliahirishwa hadi Julai 18, 2018 kwa ajili ya kutajwa.
Mpekuzi.
Comments