Upungufu Wafanyakazi, vifaa wasababisha kujifugua kwa taabu.

UPUNGUFU wa Wafanyakazi na vifaa katika wodi za wazazi pamoja na Idadi kubwa ya akinamama wanaofika katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kunapelekea matatizo kwa mama wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua.
 
Akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa kupitia Mradi wa PartoMa Daktari wa Wodi ya Wazazi wa Hospitali hiyo Dk. Natasha Housseine, alisema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na madaktari na wakunga, mapungufu hayo yanasababisha baadhi ya wakati watoto kupoteza maisha muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa kukosa uangalizi mzuri.
 
Dt. Natasha alisema Hospitali ya Mnazimmoja wastani ya watoto wachanga  12000 huzaliwa kwa mwaka idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na nyenzo na wafanyakazi waliopo ndani ya wodi.
 
Alieleza kuwa kutokana na tatizo hilo, Mradi wa PartoMa ambao unalenga kufuata taratibu zote za kumuangalia mama mjamzito tokea mwanzo wa kupata uchungu hadi kujifungua umeanzishwa miaka mitatu iliyopita katika Hospitali hiyo.
 
Alisema Mradi wa PartoMa unaotekelezwa kwa pamoja na Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na Chuo Kikuu cha Copenhagen unasaidia kutoa miongozo na mafunzo kwa madaktari na wakunga wachanga ili kuhakikisha usalama wa wazazi wakati wa kujifungua na watoto wachanga baada ya kuzaliwa.
 
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto wachanga wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja ,Dk. Salma Abdi Mahmoud, alisema Wizara ya Afya imekuwa ikifanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na madaktari wa Zanzibar, kutoka nje ya nchi  na Taasisi za Kimataifa kuhakikisha mama wajawazito na watoto wachanga wanapatiwa huduma bora wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
 
Alisema mahitaji muhimu ya mama wajawazito na watoto wachanga  hivi sasa yamesambazwa katika maeneo yote mijini na vijijini na aliwashauri akinamama  kuzitumia huduma hizo kuimarisha afya zao na watoto wanapozaliwa.
 
Zanzibarleo.

Comments