Dk. Shein: Ampa pongezi makamu.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, kwa kumsaidia kazi na kuendelea kuisimamia vyema ofisi yake.
 
Aliyasema hayo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, wakati ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2017/2018 na mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2018/2019.
 
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi Seif kwa kumsaidia kazi pamoja na kuupongeza uongozi wa ofisi hiyo na watendaji wake kwa kufanya kazi zinazoonekana na zisizoonekana zikiwemo mazingira na UKIMWi.
 
Pia, alimpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wengine wote wa ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya ikiwemo katika baraza la wawakilishi.
 
Pamoja na hayo, alisisitiza haja ya usimamizi katika utekelezaji wa majukumu ya kazi hatua ambayo huleta ufanisi mkubwa na uwajibikaji kazini.
 
Alieleza kuwa kuanzishwa kwa taasisi za utafiti ambazo zimeundwa kwa mujibu wa sheria kuna umuhimu mkubwa katika kufikia malengo yaliokwekwa juu ya suala zima la tafiti hapa Zanzibar.
 
Alisisitiza kuwa upimaji wa UKIMWI ni jambo la hiari hivyo alitoa wito kwa uongozi huo kuendelea kutumia utamaduni wa kuwashajiisha wananchi kwenda kupima badala ya kuwalazimisha.
Zanzibarleo.

Comments