Balozi Amina: Wanahabari vitangazeni vivutio vya utalii Pemba.

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Balzoi Amina Salum Ali, ameviomba vyombo vya habari kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyoko kisiwani Pemba, ili ziweze kutambulika ndani na nje ya nchi.
Alisema kisiwa cha Pemba kina sifa na hadhi ya aina ya pekee duniani, ambayo wageni na wenyeji wengi bado hawajaitambua, hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari kuifichua hadhi hiyo.
Alisema hayo wakati akifungua tamasha la utalii, utamaduni na biashara Pemba, katika uwanja wa Gombani, Chake Chake.
Alisema kisiwa cha Pemba kina vivutio vingi ikiwemo popo ambaye anapatikana kisiwani humo pekee.
Aidha ameitaka kamisheni ya utalii, kulitumia tamasha hilo kwa lengo la kukuza utalii kwa kuvitangaza vivutio vyote vya vilivyomo ndani ya Pemba.
Naye waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, alisema lengo la kuandaa tamasha hilo ni kuendeleza utalii kupitia biashara na michezo kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo kisiwani humo.
Alisema kutokana na matamasha na maonyesho yanayofanyika anaamini Pemba itabadilika katika shughuli za kitalii, hasa ikizingatiwa kuwepo kwa wawekezaji wanaojenga hoteli za kisasa.
Zanzibarleo.

Comments