Wakati
Shwaibu Jumanne akitafakari jinsi ya kuanza tena maisha uraiani, mambo
mawili bado yanamtesa baada ya kukaa mahabusu kwa miaka mitano.
Jumanne,
maarufu kwa jina la Mredii, ndiye pekee aliyeepuka hukumu ya kifo
wakati Mahakama Kuu ilipotoa hukumu dhidi ya watu sita walioshtakiwa kwa
kosa la kumuua mfanyabiashara maarufu wa Mirerani mkoani Manyara,
Erasto Msuya.
Washtakiwa
wenzake watano wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa, lakini Mredii amerudi
uraiani akitafakari maisha mapya baada ya kusimama kazi yake ya
uchimbaji madini kwa miaka mitano.
Hata hivyo, tafakuri hiyo inakabiliwa na kumbukumbu mbaya ya tukio lake; kuanzia alipokamatwa hadi maisha ya mahabusu.
“Moja
ya mambo ambayo sitakaa niyasahau ni maumivu niliyoyapata wakati
nilipokamatwa,” anasema Mrediii katika mahojiano maalumu na Mwananchi
baada ya kuachiwa huru.
“Kipigo nilichokipata mikononi mwa polisi kimemsababishia kilema na maumivu.”
Pamoja
na kwamba hakusema bayana katika mazungumzo na Mwananchi, Mredii
aliiambia mahakama wakati wa utetezi kuwa aliteswa na polisi hadi kupewa
ulemavu, ikiwamo kuhasiwa.
Kutokana
na kuhasiwa, Mredii alidai aliamua kumpa talaka mmoja ya wake zake,
aliyemtaja kuwa ni Zuhura Hassan kwa vile alikuwa hana uwezo tena kama
mwanamume. Amebakiwa na mkewe anayeitwa Adile Juma.
Akiongozwa
na wakili wake Majura Magafu kutoa utetezi wake, Mredii alidai mbali na
kuhasiwa, polisi walimvunja mara mbili mguu wa kushoto na mara moja
mguu wa kulia.
Alisema wakati fulani walimfunga kamba na kumning’iniza kama mbuzi aliyebanikwa.
“Kwa
hayo mateso niliyopata hapo kituoni nimekuwa mlemavu. Niliwekwa staili
ya mbuzi anayechomwa nikiwa sina nguo,” alidai mahakamani.
Katika
mahojiano maalumu na Mwananchi, Mredii alisema hakupata matibabu mazuri
kutokana na kipigo hicho na kwamba kwa vile sasa yuko huru, moja ya
vipaumbele vyake ni kupata matibabu sahihi ya afya yake.
Anasema
jambo jingine ambalo hatalisahau ni kulazimishwa kulala saa 9:00
alasiri na kufungiwa vyumbani hata kama huna usingizi. “Wakati mwingine
watu wako nje kwenye shughuli zao, lakini sisi tunalazimishwa kulala,”
alisema Mredii.
“Hili jambo haliwezi kutoka kwenye akili yangu kwa haraka na litanisumbua kwa muda mrefu sana.
“Kuanzia
saa 9:00 (alasiri) mtu unafungiwa ndani, unaambiwa ulale. Kwa kweli
yale yalikuwa mateso makubwa kwangu. Halafu chumba kimoja tunalala watu
18 hadi 27. Kwa kweli sitakaa niyasahau maisha haya.”
Hali hiyo ndiyo inamfanya ashauri vijana na watu wengine kutojihusisha na mambo ambayo yanaweza kusababisha wapelekwee gerezani.
“Waepuke kufanya jambo lolote litakalowafanya wapelekwe gerezani kwa kuwa kule ni mahali pa kudhalilisha sana,” anasema.
“Mtu
unapokuwa gerezani unakuchukuliwa kama mhalifu na unapokuwa kwenye lile
karandinga watu wanaona wewe ni mhalifu na wengine wanakuita mwizi bila
kujua ni kosa gani limekupeleka gerezani.
“Lipo
suala la matitabu. Mtu anapewa matibabu ya kawaida bila kujali tatizo
linalomkabili na ikitokea wakaamua kukupeleka Hospitali za Rufaa nje ya
magereza ni kwamba mtu utakuwa umezidiwa.
“Mimi
mwenyewe nimetoa matatizo yangu ikiwemo tatizo la vidonda vya tumbo,
lakini sijawahi kupimwa licha ya kuomba sana nipelekwe kwenye vipimo ili
kujua vidonda vimefikia hatua gani.
“Nimekuwa
nikitumia dawa bila kujua (kama) ndizo zinatibu. Sasa natakiwa kwenda
kwenye vipimo kwa kuwa kipindi cha miaka mitano nimekaa gerezani
(vidonda vya tumbo vimekuwa sugu hasa (kwa kuwa) kule mlo ni mmoja.”
Hukumu
ya Mredii na wenzake; Sharifu Mohamed, aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza,
Musa Mangu (wa tatu), Karim Kuhundwa (wa tano), Sadik Mohamed (wa sita)
na Ally Mussa (wa saba), ilitolewa Julai 23 na Jaji Salma Maghimbi.
Walishtakiwa
kwa mauaji ya Msuya, maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, aliyeuawa
Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Lakini
wakati Jaji Maghimbi aliwapa adhabu ya kifo washtakiwa watano,
alimuachia huru Mredii baada ya kutoridhika na hoja za kutaka atiwe
hatiani.
Jaji
Maghimbi alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka haukuweza
kuthibitisha shitaka dhidi ya Mredii, hivyo kuamua kumuachia huru.
‘Sikuhusika
kupanga wala kushiriki mauaji ya Erasto Msuya na naomba jamii inipokee”
alisema Mredii katika mahojiano na Mwananchi.
Anasema uhusiano wake na baadhi ya watu umekuwa ukimtia matatizoni na vyombo vya dola.
“Mwaka
2000 niliwahi kutuhumiwa kwa kosa la mauaji porini Mirerani lakini
baada ya upelelezi, nilionekana sikuhusika na kuachiliwa baada ya kukaa
mahabusu miezi sita,” alisema Mredii.
“Na
hii naona inaweza kusababishwa na hisia kwa kuwa hata tukio
linalonikabili naona linaweza kuwa watu wanaangalia ukaribu wangu na
watu kwa kuwa Mjeshi ni shemeji yangu.
“Sharifu
ni mfanyabiashara ambaye nimekuwa nikimpelekea mawe na hii inaweza kuwa
ndiyo iliyosababisha nikahusishwa na matatizo hayo. Lakini namshukuru
Mungu na jaji.
“Hakika
nilifurahi sana sana kuachiwa na naamini jaji alitumia waledi wake wa
kazi kwa kuona kuwa mimi sihusiki na tukio lile, na ukweli ni kwamba
mimi sihusiki.” Anasema sasa ana amani kwa kuwa yuko huru.
“Unapokuwa
huru, hata kama huna chochote unakuwa na amani. Sitamani kurudi
gerezani kwa sababu maisha kule ni magumu sana,” anasema Mredii mwenye
watato wanne.
Chanzo: Mwananchi na Mpekuzi.
Chanzo: Mwananchi na Mpekuzi.
Comments