Na Greyson Mwase, Kagera
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), kuhakikisha linakamilisha kazi ya ukarabati wa miundombinu
yote ya umeme nchi nzima kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Dkt.
Kalemani ameyasema hayo jana tarehe 10 Juni, 2018 alipokuwa
akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwenye ziara yake ya
kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme inayosimamiwa
na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) na ujenzi wa
kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji cha Rusumo kitakachokuwa na
uwezo wa kuzalisha Megawati 80 baada ya kukamilika Februari, 2020.
Alisema
kuwa, kwa sasa nchi ina nishati ya umeme wa uhakika mbali na kuwepo
kwa changamoto ya kukatika kwa umeme inayotokana na uchakavu wa
miundombinu ya kusafirisha umeme.
“Tulikubaliana
na uongozi wa TANESCO kuhakikisha kazi ya ukarabati wa miundombinu ya
umeme nchi nzima, inakamilika ndani ya miezi mitatu yaani hadi mwishoni
mwa mwezi Juni mwaka huu ili wananchi waanze kupata nishati ya umeme wa
uhakika,” alisema Waziri Kalemani.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kalemani alimtaka mkandarasi anayefanya kazi ya
ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mkoa wa Kagera kupitia Mradi wa
REA Awamu ya Tatu, kampuni ya Nakuroi Investment Company Limited
kuongeza kasi ya usambazaji katika mkoa wa Kagera ili mradi uweze
kukamilika kwa wakati na wananchi kupata umeme wa uhakika.
Aidha,
alizitaka taasisi za umma kama vile mashule, vituo vya afya na
halmashauri kutenga fedha kwa ajili utandazaji wa nyaya za mifumo ya
umeme (wiring) katika majengo yao ili waweze kuunganishiwa umeme mapema
wakati wa utekelezaji wa mradi.
Wakati
huohuo, Dkt. Kalemani aliitaka Serikali ya Mkoa na Wilaya kutenga
maeneo kwa ajili ya viwanda ili iwe rahisi kuwekewa miundombinu ya umeme
wakati wa utekelezaji wa miradi.
Awali
akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu katika mkoa
wa Kagera, Mhandisi Miradi ya TANESCO katika mkoa wa Kagera, Jackson
Kamuli alisema kuwa mradi huo ulizinduliwa mwezi Julai mwaka jana
katika kijiji cha Rwabigaga wilyani Kyerwa.
Alifafanua
kuwa, mradi huo unatekelezwa kwenye wilaya saba ambazo ni pamoja na
Bukoba Vijijini, Biharamulo, Karagwe, Kyerwa, Misenyi, Muleba na Ngara
kupitia mkandarasi ambaye ni Nakuroi Investment Company Limited ya hapa
nchini.
Alisema
mradi unatarajiwa kujenga laini za msongo wa kati wa kilovolti 33
zenye urefu wa kilomita 299.01; laini za msongo mdogo wa kilovolti 0.4
zenye urefu wa kilomita 574 na kufunga jumla ya transfoma 287.
Mhandisi
Kamuli aliongeza kuwa mradi utakapokamilika utanufaisha vijiji 141
ambapo jumla ya wateja 9,141 wanatarajiwa kuunganishwa na huduma ya
umeme.
Akielezea gharama za mradi, Mhandisi Kamuli alisema mradi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 38.5.
Wakati
huohuo akizungumza na wananchi wa vijiji vilivyopo katika wilaya za
Kyerwa, Karagwe na Misenyi mkoani Kagera, Waziri Kalemani alimtaka
mkandarasi anayetekeleza kazi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme
katika mkoa huo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambaye ni
Nakuroi Investment Company Limited kuhakikisha vijiji vyote pamoja na
vitongoji vyake vinapata umeme wa uhakika na kukamilisha kazi kwa
wakati.
Katika
hatua nyingine, Dkt. Kalemani alilitaka Shirika la TANESCO kufungua
kituo cha huduma kwa wateja katika vijiji vyote ili kuondoa kero ya
wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya umeme.
Aidha,
Waziri Kalemani aliwataka wananchi kujiandaa na huduma ya umeme kwa
kutandaza mifumo ya nyaya (wiring) kwenye nyumba zao au kuweka kifaa
kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) ili watakapofikiwa na mradi
waweze kuunganishwa mara moja.
Aliwataka
wananchi kutumia fursa zitokanazo na upatikanaji wa huduma ya umeme wa
uhakika kama kufungua viwanda kwa ajili ya mazao na mashine za
kuchomelea ili waweze kujiongezea kipato
Dkt.
Kalemani alisema umeme wa uhakika utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi
wa nchi hasa katika maeneo ya vijijini kutokana na shughuli za viwanda
vidogo vidogo na kilimo.
Mpekuzi.
Comments