Rais
wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa aliwasili Tanzania jana na kukubaliana
na Rais John Magufuli kushirikiana kibiashara, utalii na kijamii.
Sambamba na hilo, kiongozi huyo alizungumzia shambulio lililofanywa dhidi yake Juni 23, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Bulawayo nchi humo akisema lilikuwa dogo na nchi yake iko salama.
Rais
Mnangagwa alisema hayo Ikulu mjini hapa, ambapo baadhi ya wasaidizi
wake na viongozi wa chama chake cha Zanu –PF walijeruhiwa.
Katika
mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza, mwanasiasa huyo
alilihusisha tukio hilo kufanywa na kundi la G-40 ambalo ni tiifu kwa
Grace Mugabe ambaye ni mke wa Rais mstaafu, Robert Mugabe.
Mambo Matatu Waliyokubaliana
Rais
Mnangagwa aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA), saa 5:30 asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake, Rais John
Magufuli kisha kukagua gwaride la heshima na kuelekea Ikulu
yalikofanyika mazungumzo.
Akizungumza
na waandishi wa habari Ikulu, Rais Magufuli alisema wamezungumza jinsi
ya kuimarisha uchumi wa nchi hizi mbili kiuchumi tofauti na uhusiano wa
zamani uliokuwa wa kisiasa zaidi.
“Mwaka
2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa ni Sh18.3 bilioni
sawa na Dola 8.5 milioni. Mwaka 2017 biashara ilikuwa Sh21.1 bilioni
sawa na Dola za Marekani 9.5 milioni. Kuna miradi 25 ya Zimbabwe nchini
yenye thamani ya Dola 32.02 milioni ,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wamekubaliana kupitia Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) kukuza biashara.
“Ipo
mikataba ya kulegeza masharti ya kibiashara katika Sadc. Baada ya
uchaguzi ambao naamini atashinda tutaitumia kamati yetu maalumu
kuyapitia maeneo hayo,” alisema.
“Tumekubaliana
kukuza uwekezaji, nimemwambia kuna hekta 44 milioni za ardhi inayofaa
kwa kilimo na kuna hekta 29 milioni zinazofaa kwa umwagiliaji. Vilevile
kuna uwekezaji wa mifugo, uvuvi na uchakataji wa madini.”
Katika
utalii, Rais Magufuli alisema wamekubaliana kushirikiana wakitumia
wingi wa vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia na kutumia mikataba ya
mashirika ya ndege likiwamo la Fasjet.
“Mathalan,
mtalii akitoka Victoria Falls aende pia Serengeti halafu amalizie
safari yake kwenye fukwe nzuri za Zanzibar,” alisema.
Rais
Magufuli alisema pia wamekubaliana kuwa na ushirikiano katika huduma za
jamii ikiwamo elimu, afya na utamaduni na hasa katika lugha ya
Kiswahili ambayo alisema Tanzania ina walimu wa kutosha.
Rais Mnangagwa aliyewahi kuishi nchini aliishukuru Tanzania kwa kuratibu harakati za ukombozi wa Afrika.
“Dar
es Salaam tuliyoishi miaka ya 1963 na 1964 ni tofauti kabisa na ya
sasa. Tulijenga kambi ya kijeshi kule Bagamoyo ikiwa chini ya chama cha
Frelimo tukiwa nchi ya Rhodesia (sasa Zimbabwe), Zambia na Msumbiji,”
alisema.
Aliielezea
Tanzania kwa Wazimbabwe kama vile mkunga wa ukombozi. Alisema hali si
hivyo kwa nchi hiyo pekee bali pia kwa Namibia, Afrika Kusini na Angola,
hivyo ni lazima kuishukuru.
Rais
Mnangagwa alisema miaka 20 baada ya Zimbabwe kupata uhuru iliingia
kwenye anguko la uchumi kutokana na kutekeleza sera ya ugawaji ardhi kwa
watu weusi.
“Kwa
sasa tunajitambulisha katika uwekezaji wa kimataifa. Hata zile nchi
zilizojitenga baada ya kuwekewa vikwazo tunazikaribisha, lakini kwa nchi
kama Tanzania ni rafiki yetu tutaendelea kushirikiana,” alisema.
Rais Mnangagwa amepanga kutembelea iliyokuwa kambi yao ya kijeshi ya Frelimo mjini Bagamoyo mkoani Pwani leo.
Mpekuzi.
Comments