Mfalme wa Saudi Arabia ndiye atakayegharamia safari na matibabu ya pacha hao, imeeleza taarifa iliyotolewa jana na kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bandar Abdullah Al-Hazzan.
Pacha hao wenye jinsi ya kike walioungana eneo la tumboni wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu Februari.
Balozi huyo alitoa taarifa hiyo baada ya kuwatembelea pacha hao waliolazwa pamoja na mama yao, Jonisia Benatus katika jengo la wazazi.
Mama wa watoto hao alimshukuru mfalme huyo kwa kumsaidia watoto wake kupata matibabu.
“Namshukuru sana kunisaidia watoto wangu waweze kutenganishwa, naushukuru uongozi wa Muhimbili kwa msaada wao, familia yangu haikunitenga na siku zote wananiombea hilo liweze kutimia.
“Hawa ni uzao wangu wa pili, wa kwanza ni mtoto mmoja wa kiume yeye hana tatizo lolote, nilijisikia vibaya nilipoelezwa nimejifungua watoto walioungana,” alisimulia.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma na huduma kwa wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema watasafiri kwenda Saudi Arabia ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.
Aligaesha alisema kaimu balozi aliwaeleza kuwa nchi hiyo ina uzoefu wa miaka mingi katika kuhudumia pacha wa aina hiyo na kwamba, tangu mwaka 1990 hadi sasa wamefanikiwa kuwatenganisha pacha wapatao 35 kutoka nchi 14.
Naye mkurugenzi mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru alimshukuru kaimu balozi huyo kwa ujumbe huo kutoka kwa Mfalme.
“Tumekuwa na ushirikiano na Saudi Arabia kwa muda mrefu,” alisema Profesa Museru.
Comments