Dk. Shein yatangazeni mafanikio tuliyopata.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi waliyojipangia.

Dk. Shein  alieleza hayo jana ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa wizara hiyo ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka 2017/2018 na mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2018/2019.

Alisema kuna umuhimu wa kutangazwa mafanikio ya kiutendaji yaliyofanikishwa na wizara hiyo kupitia vyombo vya habari. Nao kuongeza, “Hakuna wa kuyasema mambo ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kama si siye wenyewe, mmefanya mambo mengi mazuri”,alisisitiza.

Alifahamisha umuhimu wa kutolewa mafunzo kwa lengo la kuwaandaa wataalamu watakaosadia kuimarisha sekta hizo ikiwa ni pamoja na kuendeleza ufanyaji wa tafiti ambazo ndio nguzo muhimu kwa wizara hiyo.

Dk. Shein aliwakumbusha viongozi wa wizara hiyo umuhimu kwa viongozi kuwa wasikivu na kukaribisha ushauri, kwani viongozi huwatumikia wananchi hivyo ni vyema kusikilizwa matatizo yao na kuepuka kukaa ofisini hasa kwa maumbile ya sekta hizo.

Aidha alieleza kuwa zoezi la bango kitita limeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza na kutekeleza mipango yote muhimu inayopangwa na wizara za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awali waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma alieleza kuwa sekta ya kilimo ikijumuisha mazao ya mifugo, uvuvi na misitu bado inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Aidha, alieleza kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hii ambayo imeongoza kwa ukuaji katika pato la Taifa na kufikia wastani wa asilimia 8.8 mwaka 2017 kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 3.6 wa mwaka 2016.

Aliongeza kuwa mwaka 2017 sekta ya kilimo imekuwa ya pili kuchangia pato la taifa kwa wastani wa asilimia 27.9 ikilinganishwa na asilimia 25.5 mwaka 2016.

Zanzibarleo.

Comments