Wabunge waibana Serikali bungeni kuhusu nyongeza ya mishahara.

Wabunge wa CCM, Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini) na Mussa Sima (Singida Mjini) wameitaka Serikali kutoa majibu ya lini wafanyakazi wataongezewa mishahara ili kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Wabunge hao wamehoji hayo leo Mei 2, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati wakiomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge wakitumia kanuni ya 67 (8) baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Mapunda amesema; “…kwa kuwa kuondoa umaskini wa kipato, kuna uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa Serikali wa pande zote. Na kwa kuwa jana siku ya Mei Mosi Rais (John Magufuli) aliji ‘commit’ kuwa ongezeko la mishahara pamoja na mambo mengine litazingatia hali halisi ya uchumi, uwezo wa taifa na uwezo halisi wa Serikali.”

“Na kwa kuwa ameji ‘commit’, Serikali inatoa kauli gani lini mishahara hiyo itapanda kwa sababu suala hili jana limeacha sintofahamu kwa wananchi,” ameongeza:

Naye Sima licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa hotuba aliyoitoa jana mjini Iringa amesema; “Lakini kama bunge, tungetaka kujua ni lini sasa watumishi hawa watapandishiwa mishahara.”

Akitoa majibu ya miongozo hiyo ya wabunge, Chenge amesema jana hata yeye alimsikiliza vizuri Rais Magufuli akielezea suala hilo.

 Chenge amesema:  “Rais alisema hali ikiwa nzuri ataongeza mshahara na ataongeza kikweli kweli. “
Mpekuzi.

Comments