Serikali
imefanya marekebisho ya utumishi wa umma sura 298 kuongeza umri wa
kustaafu kazi maprofesa na wahadhiri waandamizi katika vyuo vikuu vya
umma.
Wengine watakaohusika ni madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu katika hospitali za umma nchini.
Hiyo
ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ambayo imesainiwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Makwaia Makani.
Taarifa
hiyo inasema umri wa kustaafu kazi kwa madaktari katika hospitali za
umma ni miaka 60 badala ya 55 kwa hiari na miaka 65 badala ya 60 kwa
mujibu wa sheria.
“Katika
kukabiliana na upungufu wa wanataaluma na wataalamu waliopo kwa sasa
katika vyuo vikuu vya umma na hospitali za umma nchini.
“Serikali
imefanya marekebisho katika sheria ya utumishi wa umma sura 298
kuongeza umri wa kustaafu kazi maprofesa na wahadhiri waandamizi katika
vyuo vikuu vya umma na madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu katika
hospitali za umma kupitia sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali
Namba 1 ya Mwaka 2008.
“Marekebisho
yaliyofanywa katika sheria ya utumishi wa umma yameainisha umri wa
kustaafu kazi kwa kada tajwa hapo juu kwa miaka 60 badala ya 55 kwa
hiari na miaka 65 badala ya 60 kwa mujibu wa sheria. Mabadiliko haya
yameanza rasmi Februari 9 mwaka huu,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo ilisema madaktari bingwa wote ambao hawakuwa wamefikisha umri wa
kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria Februari 9 mwaka huu, wataendelea na
ajira zao hadi hapo watakapofikisha miaka 65 na kwamba taarifa zao za
kustaafu kwa wale waliopata zinafutwa.
Vilevile
taarifa hiyo ilieleza kuwa madaktari bingwa watakaotaka kustaafu kwa
hiari watatoa taarifa ya maandishi kwa mkurugenzi mtendaji.
Alipoulizwa
kuhusu taarifa hizo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma
kwa Wateja, Aminiel Aligaesha alisema ni kweli tangazo hilo ni la kwao.
Kuanza
kwa sheria hiyo kunatokana na kupitishwa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria mbalimbali Namba Tano wa Mwaka 2017 ambao utazihusisha sheria
tano ikiwamo ya Utumishi wa Umma sura namba 298 ambako kifungu kipya cha
25A kitaongezwa.
Vikao
vya kamati za Bunge vimeanza huku miongoni mwa miswada itakayojadiliwa
ikiwa ni ule utakaoongeza umri wa kustaafu kwa lazima kutoka miaka 60
hadi 65 kwa maprofesa, wahadhiri waandamizi na madaktari bingwa wa
magonjwa ya binadamu wa umma.
Inaelezwa
kuwa lengo la kuongezwa kwa sheria hiyo ni kuweka kwenye masharti ya
umri wa kustaafu kwa watumishi wa umma ambayo hayapo kwenye sheria ya
sasa.
Mfumo
huo mpya unalenga kuongeza umri wa kustaafu wa utumishi wa umma kwa
ridhaa kwa maprofesa na wahadhiri waandamizi wa vyuo vikuu vya umma na
madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu wa hospitali za umma ili uwe 60
kwa wale wanaostaafu kwa hiari badala ya 55 wa sasa.
Pia, mfumo huo unalenga kuongeza umri wa kustaafu kwa lazima uwe miaka 65 badala ya sasa wa miaka 60 ya sasa.
“Marekebisho
haya yanalenga kutekeleza uamuzi wa Serikali unaolenga kuongeza umri wa
kustaafu kwa maprofesa, wahadhiri waandamizi wa madaktari bingwa wa
binadamu kutoka vyuo vikuu vya umma na hospitali za umma,” ilielezwa.
Mpekuzi.
Comments