SMZ yaahidi kuthamini na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuthamini na  kulinda uhuru wa vyombo vya habari ili kuwawezesha waandishi wa habari kufanya kazi zao Nchini.

Akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusiana na siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari katika Ukumbi wa Wizara ya habari Kikwajuni Mjini Zanzibar,Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya kale Mahamoud Thabit Kombo amesema Serikali inatambua umuhimu wa vyombo vya habari hivyo itaendelea kutoa taarifa  ili kuwawezesha wananchi kunufaika na haki  zao za msingi.

Amesema wananchi wanahitaji kujua taarifa mbalimbali kuhusiana na Nchi hivyo waandishi wa habari watakapopewa taarifa kwa wakati wataweza kuisaidia jamii na serikali kwa ujumla.

Waziri kombo  amewataka Waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi zao kwa kufuata Sheria na Maadili ya Kazi zao ili kujiepusha na matatizo ambayo yaweza kuondoa amani ya Nchi.

Hata hivyo amesema Serikali haitamvumilia Mwandishi  au Chombo Chochote kitakachojihusisha na utoaji wa taarifa ambazo zitaleta athari katika jamii ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao na Nchi kuendelea kubaki katika hali ya amani na Usalama.

Madhimisho ya Siku ya Vyombo vya Habari  huadhimishwa kila ifikapo may 3 ya kila mwaka ambapo kwa Zanzibar yanatarajiwa kuadhimishwa katika Ukumbi wa Wawakilishi la Zamani yakiwa na ujumbe usemao WAJIBU WA UONGOZI ,VYOMBO VYA HABARI HAKI NA SHERIA.

Zanzibar24.

Comments