Mkurugenzi
mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Leodegar Tenga
amesema baadhi ya wenye viwanda wana hofu ya kushiriki shindano la
mzalishaji bora wa mwaka wakidhani wataharibu masoko yao iwapo
hawatashinda.
Hata
hivyo, Tenga aliwatoa hofu kwamba tuzo hizo hazina uhusiano wa moja kwa
moja na ubora wa bidhaa, bali wanaangalia vigezo vingine muhimu katika
uzalishaji na namna wenye viwanda wanavyoweza kujifunza kutoka kwa
wenzao.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema katika tuzo za Rais za
mzalishaji bora wa mwaka 2017 zinazotarajiwa kufanyika Mei 4, ni wenye
viwanda 36 waliojitokeza kushiriki shindano hilo.
Tenga
alibainisha kuwa mwitikio umeongezeka kidogo ikilinganishwa na mwaka
jana, lakini akasisitiza kwamba kampuni kubwa hazitaki kushiriki kwa
kuhofia kuharibu taswira iwapo hazitashinda.
“Changamoto
kubwa ni hawa wazalishaji wakubwa, ukiwafuata wanakwambia hawatashiriki
wakihofia kuharibu taswira za kampuni zao,” alisema Tenga na kuongeza:
“Tunajitahidi
kuwaeleza kuwa mashindano hayo ni muhimu kwao na hayahusiani na ubora
wa bidhaa zao hivyo wanatakiwa kushiriki kuonyesha ukuaji wa uzalishaji
wao.”
Awali,
mwenyekiti wa CTI, Dk Samwel Nyantare alisema kwamba tuzo hizo
zitatolewa kwa sekta 17 zinazotambulika kimataifa na mwaka huu
wameongeza sekta moja ya matumizi bora ya nishati.
Alizitaja
baadhi ya sekta zitakazoshindaniwa kuwa ni vinywaji, ujenzi, kemikali,
nishati, plastiki, fedha, mbao na samani, chuma, magari, usafirishaji,
karatasi, dawa na vifaatiba, nguo na bidhaa za madini.
Naye
mkurugenzi wa machapisho na mawasiliano wa CTI, Thomas Kimbunga
alibainisha kuwa vigezo vilivyotumika kuwapata washindi wa kila sekta ni
pamoja na utendaji wa kiuchumi, utendaji wa kiteknolojia, matumizi ya
nishati, uuzaji bidhaa nje ya nchi, usalama sehemu ya kazi na kuzingatia
masuala ya kijamii.
Kuhusu
mshindi wa jumla, Kimbunga alisema kwamba wataangalia vigezo vingine
kama mizania ya jinsia kwenye ngazi ya utawala, uhifadhi wa mazingira,
uhusiano mzuri, kuzingatia viwango vya ubora na uhusiano na sekta
nyingine za uchumi.
Mpekuzi.
Comments