Manispaa mjini kukusanya 7.6bn/-

BARAZA la Manispaa Mjini linakadiria kukusanya shilingi bilioni 7.65 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 18.3 kutoka mwaka 2017/2018.
Mkurugenzi wa baraza hilo, Aboud Hassan Serenge alieleza hayo alipokuwa akizungumza na muandishi wa habari ofisini kwake Malindi mjini Unguja.
Serenge alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 4.66 zinakadiriwa kukusanywa kupitia vyanzo vya ndani ambazo ni ongezeko la asilimia 32 kutoka bajeti iliyopita na shilingi bilioni 2.5 zitaingia kama mishahara kutoka serikali kuu na shilingi milioni 492 zitaingia kama ruzuku ya ugatuzi ambazo kwa pamoja vinajulikana kama vyanzo nje vya mapato vya baraza hilo.
“Baraza la Manispaa mjini tuna vyanzo viwili vya mapato, moja ni mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani na pili tunategemea kutoka vyanzo vya nje. Kwa mwaka wa fedha 2018/19 tunarajia kukusanya shilingi bilioni 4.66 kutoka vyanzo vya ndani na shingi bilioni 2.5 mishahara kutoka serikali kuu na milioni 492 katika sekta zilizogatuliwa”, alifafanua mkurugenzi huyo.
Akifafanua makadirio ya matumizi ya baraza hilo, Serenge alisema kuwa baraza litatumia shilingi bilioni 2.3 kwa programu ya utekelezaji wa maendeleo ya jamii ambayo inajumuisha shughuli za usafi na upendezeshaji wa mji kiuchumi na kiuzalishaji na shilingi bilioni 5.0 zitatumika katika program ta utawala na uendeshaji.
Serenge alisema kuwa katika kufikia malengo ya makadirio hayo mikakati madhubuti imewekwa ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieloktroniki, ufuatiliaji na tathmini ili kugundua kasoro za utekelezaji wa bajeti, kuengeza wafanyakazi wenye sifa na kuwajengea uwezo wafanyakazi waliopo.
Mkurugenzi huyo aliitaja mikakati mengine kuwa ni kuengeza mashirikiano na miji mengine duniani, kuengeza ushirikishwaji wa wananchi na kuimarisha sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za baraza na ukusanyaji wa mapato.
Katika hatua nyengine Serenge aliwataka madiwani wa wadi za manispaa ya mjini kuengeza mashirikiano na watendaji wa baraza hilo ili kuweza kufikia lengo.
Aidha aliwataka watendaji wa baraza hilo kufanyakazi kwa weledi na kua na tabia ya kutunza takwimu ili kuawa na majibu sahihi jambo ambalo litawafan ya wajumbe wa baraza hilo kuwa na imani nao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Zanzibarleo.

Comments