Jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Karume yaipa hofu SMZ.

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud, amesema ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume (terminal 3) utakapokamilika, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 2.5 kwa mwaka.

Alisema kwa sasa uwanja huo unahudumia abiria milioni 1.8.

Aliyasema hayo wakati akifanya ziara ya kuangalia muendelezo wa ujenzi wa jengo hilo.
Alisema ameridhishwa na hali ya ujenzi inavyoendelea kwani kuna vitendea kazi vya kutosha ikiwemo kokoto na tani 15,000 za mchanga.

Hata hivyo, alisema changamoto iliyopo ni namna ya kuliendesha jengo lenyewe litakapomalizika kwa sababu litakuwa kubwa hivyo linahitaji wataalamu wengi wenye ujuzi.

“Jengo hili ni kubwa na linahitaji umeme mwingi kwa sababu kutakuwa na ngazi za umeme, lifti na viyoyozi,” alisema.

Akizungumzia uwezo wa kiutendaji, alisema kutahitajika wafanyakazi wenye uwelewa na wenye leseni na wanaofamu wanachokifanya.

Hivyo aliwataka vijana kusoma kwa bidii kwani serikali inahitaji wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali nchini ikiwemo viwanja vya ndege.

Zanzibar24.

Comments