Uamuzi huo utatolewa na Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla kufunga ushahidi. Iwapo Jaji Maghimbi ataona yupo mshtakiwa ambaye hana kesi ya kujibu atamwachia huru, lakini kwa watakaoonekana wana kesi ya kujibu, itawalazimu kujitetea.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Mussa. Awali, upande wa mashtaka ulieleza ungekuwa na mashahidi 50 lakini hadi ulipofunga ushahidi Ijumaa iliyopita, walileta mashahidi 27 na vielelezo 27 viliwasilishwa mahakamani. (Daniel Mjema)
Comments