Siku
chache baada ya mkazi wa Tarime, Suguta Chacha kufariki dunia akiwa
mikononi mwa polisi, familia yake imekataa kupokea msaada wa chakula
kilichotolewa na ofisi ya kamanda wa polisi, Kanda Malumu ya
Tarime/Rorya.
Chakula
hicho kilitolewa na jeshi hilo kwa ajili ya shughuli za msiba wa Suguta
ambaye ni ndugu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliyefariki
Aprili 27 akiwa mikononi mwa polisi.
Msaada
huo wa kilo 100 za mchele, unga kilo 100, maji ya kunywa katoni 20
pamoja na sukari uliwasilishwa msibani hapo na Kamanda wa Polisi wa
kanda hiyo, Henry Mwaibambe lakini ulikataliwa.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo Kamanda Mwaibambe alisema: “Tuliache kwa sababu halina maana tena na tunapenda liishe salama.”
Katibu
wa ukoo wa Suguta, Chacha Heche alisema familia hiyo iko tayari kupokea
msaada wa Kamanda Mwaibambe kama mtu binafsi kutokana na jinsi
alivyoshirikiana nao tangu mauaji hayo yatokee, lakini haitapokea msaada
wa polisi kama taasisi.
“Tutapokea
msaada kutoka kwa yeyote mwenye mapenzi mema lakini siyo taasisi ya
Jeshi la Polisi. Tayari tumechanga zaidi ya Sh5 milioni kati ya Sh8
milioni zinazohitajika kugharamia mazishi ya ndugu yetu,” alisema Heche.
Alisema
familia inaheshimu na kutambua jinsi Kamanda Mwaibambe
anavyoshughulikia tukio hilo na itashirikiana naye na kumkaribisha
katika mazishi kama mtu binafsi na siyo kwa kofia ya polisi.
Katibu
huyo wa ukoo wa Suguta, alisema marehemu atazikwa kesho baada ya ndugu
kujiridhisha na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi.
Suguta anadaiwa kufariki dunia baada ya kuchomwa visu na askari polisi, William Marwa (50).
Marwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime juzi na kusomewa shtaka la mauaji.
Mwendesha
Mashtaka wa Polisi, Mwani Mrisho alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo
Aprili 27 ambako alimuua Suguta (27) kwa kumchoma na kisu.
Tukio
hilo lilitokea usiku wa siku hiyo baada ya Suguta na mmiliki wa baa
kukamatwa na polisi waliokuwa doria. Hata hivyo, ndugu wa Suguta
walipokwenda kumuangalia siku inayofuata waliambiwa amefariki na mwili
upo mochwari.
Mpekuzi.
Comments