
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzingagwa
Mchany ilisema bei hizo mpya zitatumika Tanzania Bara kuanzia leo.
Mchany alisema mabadiliko hayo ya yanatokana na kushuka kwa bei ya
mafuta katika soko la dunia na marekebisho ya bei yaliyofanywa na Ewura
kutokana na kubadilika kwa tozo za wakala na Serikali za mitaa katika
bidhaa hizo.
Ikilinganishwa na tangazo la bei ya mafuta la Aprili 4 kwa mafuta
yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam, bei ya petroli imepungua
kwa Sh88 kwa lita (asilimia 3.8) na dizeli Sh61 kwa lita (asilimia
2.75); huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Sh2 kwa lita sawa na
asilimia 0.09.
Tofauti na wanunuzi wa rejareja, bei ya wale wa jumla upande wa
petroli imepungua kwa Sh100.91 kwa lita (asilimia 4.58), dizeli Sh73.71
kwa lita (asilimia 3.52) na mafuta ya taa Sh10.49 kwa lita sawa na
asilimia 0.51.
Mafuta yanayopita Bandari ya Tanga bei kwa wanunuzi wa rejareja
imeongezeka kwa asilimia 0.14 kwa petroli na asilimia 0.71 kwa dizeli.
Lakini wauzaji wa jumla bei imepungua kwa asilimia 0.46 (Sh9.8 kwa
lita) kwa petroli na asilimia 0.1 (Sh1.9 kwa lita) kwa dizeli.
“Hakuna uingizaji mpya wa mafuta uliofanyika nchini kupitia Bandari
ya Tanga, lakini kutokana na mabadiliko ya bei ya Ewura kuna mabadiliko
ya bidhaa hizo tofauti na ilivyotangazwa Aprili 4,” alisema Mchany na
kuongeza:
“Bei ya petroli itaongezeka kwa Sh3 kwa lita, huku dizeli ikiongezeka kwa Sh15 kwa lita.”
Kutokana na kupungua kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Tanga, Ewura
imewashauri watumiaji wa mikoa ya Nyanda za Juu kuchukua bidhaa hiyo
katika Bandari ya Dar es Salaam kwa bei elekezi.
Taarifa ya Mchany inasisitiza kila kituo cha kuuzia mafuta kuchapisha
bei kwenye mabango yanayoonekana bayana na kituo kutoa risiti za
kielektroniki (EFD) kwa kila mauzo.
Zanzibar24.
Comments