Waumini
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Mashariki na Pwani(DMP), walisomewa barua maalumu kuhusiana na suala
la Askofu wao, Dk. Alex Malasusa.
Kusomwa
kwa barua hiyo jana kunatokana na kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi
ya Mashariki na Pwani kilichokutana Jumatano iliyopita.
Barua
hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Godfrey Nkini,
ilisomwa katika usharika mbalimbali za dayosisi hiyo wakati wa
matangazo.
Kwa
mujibu wa barua hiyo, washarika wametakiwa kufahamu kwamba Dk. Malasusa
ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani na dayosisi itaendelea na
umoja na mshikamano na askofu huyo katika kuongoza na kuihubiri injili
ya Yesu Kristo.
“Halmashauri kuu inaendelea kulifuatilia jambo hili kwa makini. Washarika mnaombwa kuwa watulivu na kuliombea kanisa.
“Tunaombwa kutunza amani na umoja wa kanisa kama neno la Mungu linavyosema,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Askofu
Malasusa, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomon Massangwa na
Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki, Dk. Lucas Mbedule, wanatuhumiwa
kwa usaliti kutokana na uamuzi wao wa kuzuia waraka wa Pasaka
ulioandaliwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo usisomwe katika dayosisi
wanazoziongoza.
Jumapili iliyopita Askofu Mbedule alilazimika kuomba radhi kutii maagizo ya Baraza la Maaskofu wa KKKT.
Waraka
huo ulioandaliwa mwishoni mwa Machi mwaka huu, wiki moja kabla ya
maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka, ulichambua masuala ya jamii, uchumi,
maisha ya siasa, umuhimu wa katiba mpya na matukio yaliyo kinyume na
kile walichokiita tunu na misingi ya taifa.
Licha
ya barua hiyo ya kanisa kusomwa baadhi ya waumini walihoji hatua hiyo
kutokana na kutosomwa na waraka wa kanisa wa Pasaka na badala yake
wamesomewa barua ya kumkingia kifua Askofu Malasusa.
Hatua
ya halmashauri kuu ya dayosisi hiyo imeonyesha kumkingia kifua kutokana
na barua iliyoandaliwa na chombo hicho na ilisomwa jana.
Kwa
mujibu wa nakala ya barua hiyo , Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo,
imesema haikuwa na lengo la kupingana na maazimio ya Mkutano Mkuu wa
Baraza la Maaskofu wa KKKT juu ya kusomwa kwa Waraka wa Pasaka.
Barua
hiyo imesema maelekezo yote yaliyotolewa yamezingatiwa na imesisitiza
kuwa umoja na mshikamano kwa Askofu Dk. Malasusa utaendelea katika
kuongoza na kuihubiri Injili ya Yesu Kristo.
Barua
hiyo ilieleza kuwa halmashauri hiyo ilikaa kikao Mei 2, mwaka huu na
ilijadili na kujiridhisha kuhusu barua aliyoandikiwa Askofu Malasusa
kuwa alikiuka mapatano yaliyotolewa na mkutano wa maaskofu wa KKKT.
“Halmashauri
Kuu imetafakari kwa kina jambo hili na kujiridhisha kwamba: Haikuwa
lengo la DMP kupingana na maazimio ya Mkutano wa Maaskofu daima.
Maelekezo yote yaliyotolewa na KKKT Makao Makuu yamezingatiwa.
“Hata
hivyo, Halmashauri Kuu imesikitishwa kwa jinsi suala zima lilivyotunzwa
hadi kufikia vyombo vya habari na baadhi yao kupotosha ukweli wa suala
zima,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Kuhusu
Askofu Malasusa barua hiyo ilisisitiza: “Washirika mfahamu kwamba
Malasusa ni Askofu wa DMP. Halmashauri inatoa pole nyingi kwa Baba
Askofu na familia yake kwa usumbufu uliojitokeza. DMP itaendelea na
umoja na mshikamano na Askofu Malasusa katika kuongoza na kuhubiri
Injili ya Yesu Kristo.”
Pamoja
na barua hiyo kutoa pole kwa washirika wote kutokana na kuumizwa kwao
na taarifa za kuandikiwa barua Askofu Malasusa za kukiuka mapatano ya
Baraza la Maaskofu, ilizodai haikuwa lengo la KKKT Makao Makuu kuwaumiza
waumini wake, pia ilieleza inaendelea kulifuatilia jambo hilo kwa
makini.
Pia barua hiyo iliwaelekeza washirika hao kuwa watulivu na kuliombea kanisa na kutunza amani na umoja.
Uamuzi
wa kumtenga Askofu Malasusa ulifikiwa na kikao cha Baraza la Maaskofu
wapatao 25, lililoketi mjini Arusha, chini ya kiongozi wake ambaye ndiye
mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Fredrick Shoo.
Mpekuzi.
Comments