Waziri Mkuu wa Iraq: Iraq iliyo imara haitaruhusu DAESH warudi tena nchini.

Waziri Mkuu wa Iraq: Iraq iliyo imara haitaruhusu DAESH warudi tena nchiniWaziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi amesisitiza kuwa, kwa kutegemea umoja na mshikamano wake na uwezo wa wapiganaji na wanachi wake, Iraq haitaruhusu magaidi wa DAESH (ISIS) warudi tena nchini humo.

Al-Abadi ameyasema hayo alipohutubia mkutano wa 10 wa jumuiya ya kimataifa ya asasi na mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini uliofanyika mjini Baghdad.
Waziri Mkuu wa Iraq amesema: "Mwaka 2014, dunia ilidhani kwamba Iraq imefika ukingoni, lakini nchi hii ililishinda kundi la kigaidi la Daesh na kurejesha tena nguvu na umoja wa ardhi yake."
Haidar Al-Abadi amesisitiza kuwa, kama si juhudi za kujitolea za wananchi, Iraq isingepata mafanikio hayo na kuongeza kwamba: ushindi dhidi ya Daesh ulitokana na umoja wa Wairaqi; na ushindi huo umeweza kuiokoa Iraq na makundi ya watenda jinai na ya kigaidi.
Waziri Mkuu wa Iraq amebainisha pia kwamba serikali ingali imefungamana na ahadi yake ya kuwarejesha wakimbizi kwa hiari yao sambamba na kukabiliana na hatua zozote zile za Daesh za kutaka kubadilisha demografia na muundo wa idadi ya watu.
Desemba 2017, Haidar al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq na Kamanda Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi alitangaza rasmi kukombolewa ardhi yote ya nchi hiyo kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi  na ukufurishaji la DAESH (ISIS)..
chanzo:parstoday.

Comments