WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa mkoa wa Mwanza kuendelea na
usaji wa wanunuzi wa zao la pamba na wawape fursa ya kuchagua maeneo
wanayotaka kununua pamba.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Aprili 01, 2018) alipozungumza na
viongozi mkoa wa Mwanza baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa
Mwanza akiwa njiani kuelekea mkoani Geita.
Waziri
Mkuu leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuwasha mwenge
wa Uhuru zitakazofanyika mkoani Geita. Kauli mbiu ya mbio za mwenge kwa
mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya
Taifa letu.’
Waziri
Mkuu alisema wakati viongozi hao wakiendelea na usajili wa wanunuzi wa
pamba ni vema wakawapa nafasi ya kuchagua maeneo watakayohitaji kukunua
kwa sababu yanaweza kurahisishia usafirishaji.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwasisitiza viongozi hao kuendelea kusimamia na
kufuatilia maendeleo ya zao hilo kwa umakini zaidi ili kuweza kubaini
changamoto zitakazojitokea na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Alisema
kutokana na mwenendo wa hali ya hewa mwaka huu wakulima wa zao la pamba
wanatarajiwa kuvuna pamba nyingi, hivyo ni vema ukatengenezwa utaratibu
utakaomrahisishia mkulima kutoa mazao shambani na kufikisha mnadani.
Waziri
Mkuu alisema utaratibu huo wa kutoa mazao shambani na kupelekwa mnadani
kwa wakati ni muhimu kwa sababu utasaidia katika kulinda pamba ili
isipoteze ubora wake.
Zao
la pamba ni miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo Serikali
imeamua kuyapa kipaumbe kwa kuyafuatilia kuazia hatua za awali za
utayarishaji wa mashamba, pembejeo pamoja na uuzaji. Mengine ni korosho,
chai, kahawa na tumbaku.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, APRILI 02, 2018.
chanzo:mpekuzi.
Comments