Waziri Mkuu awataka wanaoishi bondeni kuhama.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwa kuwa mvua inaponyesha wanapata maafa makubwa.
Akizungumza bungeni leo  Aprili 19 , katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo, amesema mara nyingi Serikali imekuwa ikiwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama lakini suala hilo utekelezaji wake  umekuwa ukiathiriwa na siasa.
“Wabunge mmekuwa mashahidi jambo hili linapoamuriwa kuna siasa zina kuwa zikizungumzwa. Ila Serikali mara kadhaa imekuwa ikiwataka wanaoishi mabondeni kuhama ili kujiepusha na madhara wanayoweza kuyapata mvua ikinyesha,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amewapa pole walioathirika na mvua na waliofariki dunia na kubainisha kuwa kamati za maafa zitafanya tathimini na miundombinu inayosimamiwa na serikali itarejeshwa katika hali yake ya kawaida.
Amelieleza Bunge kuwa Wakala wa Barabara (Tanroads) utafanya tahmini na kurejesha miundombinu katika hali ya kawaida.
“Kwa sasa mvua zinaendelea na kila mkoa kuna kamati za maafa ambazo, zitatengeneza miundombinu iliyoharibika ikiwamo barabara na maeneo mengine,” amesema.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Temeke (CUF) Abdallah Mtolea, aliyetaka kujua serikali imejipangaje kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua.
Mwananchi.

Comments