Wazanzibar washauriwa kujiunga na miradi ya maendeleo kujikwamua na umasikini.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema wananchi wa kipato cha chini wanaweza kujikwamua na umasikini iwapo watatumia vyema miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa kusaidia kaya Maskini TASAF.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani baada ya mkutano wa kufanya tathmini ya mradi wa kusaidia kaya Masikini TASAF hapa Zanzibar,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa pili wa Raisi Mhe. Muhammed Aboud Muhammed, amesema katika kipindi cha miaka mitatu  ijayo wananchi wanaonufaika na mradi huo watakuwa na uwezo wa kuiwezesha serikali kufikia Uchumi wa kati.
Amesema uwepo wa mradi huo umewawezesha wananchi kuanzisha miradi mbali mbali ya kujikwamua na umaskini ikiwemo  kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuwa na uwezo wa kuwasomesha watoto wao ambapo awali walikuwa wakikosa elimu.
 Aidha Mhe. Aboud ametoa wito kwa Wananchi wanaonufaika na mradi huo kuthamini Mchango wa Serikali na Wadau wa Maendeleo na badala yake watumie vyema fedha wanazopewa katika kuanzisha Miradi ya maendeleo itakayowaingizia kipato cha kuweza kuendeleza familia zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa Mradi wa Tasaf Chiku Thabit amesema Muamko wa wananchi kuanzisha miradi ya maendeleo umekuwa mzuri na kusababisha watoto wanaoishi katika kaya masikini kuweza kunufaika na haki zao za msingi ikiwemo kupata matibabu, elimu na malezi bora.
 Amesema katika awamu nyengine walengwa ambao wameshakuwa na uwezo wa kumudu maisha yao watatolewa katika Mradi huo pamoja na kuwezeshwaa kifedha za kuweza kuendeleza miradi yao ili kuwapa fursa wanakaya wengine kunufaika na Mradi huo.
“hawa wanakaya watakaotolewa tutawawezesha kwa kuwapa lakin tano kwa kila kaya ili ziwasaidie kuendeleza miradi yao itakayowaletea maendeo na kuwaingizia kipato”
Nae Mwakilishi wa benki ya Dunia anaesimamia masula ya Tassaf nchini Tanzania Muderis Abdullahi Mohammed,amesema ameridhishwa kuona wananchi wengi wanaonufaika na mradi huo tayari wameshanza kuondoka na Umaskini.
Zaidi ya kaya mia mbili zinanufaika na Mradi wa kusaidia kaya masikini TASAF hapa Zanzibar ili kuwawezesha wananchi kujikwamua na umasikini ambapo tangu  kuanza kwa mradi huo zaidi ya shilling Billion kumi zimetumika katika kusaidia kaya hizo na tayari wanakaya  wamekuwa na muamko wa kuanzisha miradi ya kuwapatia kipato cha uhakika.
chanzo:Zanzibar24.

Comments