Wapalestina wengine 50 wajeruhiwa na wazayuni katika siku ya tatu ya maandamano ya "Haki ya Kurejea".

Wapalestina wengine 50 wajeruhiwa na wazayuni katika siku ya tatu ya maandamano ya Wapalestina 50 wameshambuliwa na kujeruhiwa na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika maandamano yaliyoendelea kwa siku ya tatu mtawalia hapo jana yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea".

Wapalestina wasiopungua 17 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,400 wamejeruhiwa na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano hayo siku ya Ijumaa.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina kimetangaza kuwa katika makabiliano hayo ya jana pia, askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni waliwafyatulia risasi na mabomu ya kutoa machozi Wapalestina na kusababisha vijana 50 wa Kipalestina kujeruhiwa na kupaliwa na pumzi.
Wakati huohuo, Yoav Mordechai, mratibu wa utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu ametangaza kuwa maiti za mashahidi wawili wa Kipalestina waliouawa siku ya Jumamosi zitajumuishwa na maiti nyengine 24 za Wapalestina waliouawa katika vita vya mwaka 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza na wala hazitarejeshwa kwa familia zao.
Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina zingali zinaendelea chini ya kivuli cha uungaji mkono wa kila hali wa Marekani na msimamo legevu wa baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Imarati (UAE) kuhusiana na suala la Palestina sambamba na kutowajibika jumuiya za kimataifa na za kieneo. 
Hali hiyo imepata nguvu zaidi tangu Donald Trump aliposhika madaraka ya kuwa rais mpya wa Marekani.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa tangu tarehe 6 Desemba mwaka 2017 wakati Trump alipoitangaza Quds tukufu kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Wapalestina 52 wameshauwa shahidi kwa kupigwa risasi na Wazayuni na wengine zaidi ya 9,000 wamejeruhiwa.
chanzo:parstoday.

Comments