Juzi akifungua warsha ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, iliyoshirikisha wanahabari, wataalamu wa afya na viongozi wa dini, Makonda alisema atatumia wataalamu wa afya kupima ugonjwa huo ili kukabiliana na tatizo hilo katika mkoa wake.
Kina baba waliohojiwa jana kuhusu suala hilo baadhi walipongeza wakisema itasaidia kujua afya zao lakini wengine walisema ni lazima elimu itolewe kwanza kabla ya upimaji na kutaka liwe jambo la hiari.
Pia walishauri kutengwa eneo maalumu kwa ajili ya mchakato huo kuliko kufanyika kwenye makazi yao.
Mkazi wa Tabata Segerea, Gumbo Hussein alisema kampeni hiyo ni nzuri kwa sababu itasaidia wanaume kujua afya zao kwa sababu watakuwa wanafuatwa katika makazi yao tofauti na kuambiwa waende sehemu fulani kwa ajili kupima.
“Baadhi ya Watanzania hatuna desturi ya kuangalia afya zetu mara kwa mara. Ikitokea kuna eneo maalumu limetengwa kwa ajili ya watu kuangalia afya zao ni wachache wanaopata nafasi ya kuwaona madaktari kutokana na wingi wetu. Lakini hii kampeni unafuatwa nyumbani kwako ni jambo la kupongeza,” alisema Hussein.
Alisema ni hatua nzuri kampeni hiyo kufanyika nyumba kwa nyumba, lakini akatoa angalizo la kutaka utaratibu utakaotumika uwe mzuri na usiwe wa kudhalilishana kwa kuwa kampeni hiyo inalenga kujali afya za wanaume.
Lakini mkazi wa Ilala Shaaban Juma alitofautiana na Hussein akisema hatua hiyo ni nzuri lakini isifanyike nyumba kwa nyumba, bali kutengwe eneo maalumu kwa ajili hiyo.
“Wanaume wataona aibu kwa sababu wengine wanaishi na watoto na yapo maneno yanasemwa semwa kuwa tezi dume inapimwa kwa kidole, sasa hii si aibu kwa watoto wetu? alihoji Juma.
Hata hivyo, katika warsha hiyo mkuu wa mkoa huyo, aliwatoa hofu wanaume wa kuwa hawatapimwa kwa kutumia vidole, bali kwa kuchukuliwa sampuli ya damu.
Juma alisisitiza kuwa hawapingani na kampeni hiyo, bali namna itakavyotekelezwa ndio inawapa shida kuunga mkono mchakato huo.
Maganga Nsimba, ambaye pia ni mkazi wa Tabata Kisiwani aliungana na Juma kutaka kampeni hiyo ifanyike katika eneo maalumu na siyo nyumba kwa nyumba huku akimtaka Makonda kufafanua namna atakavyotumia sampuli kupima ugonjwa huo.
“Tumesikia na tumesoma kwenye baadhi vyombo vya habari mkuu wa mkoa akinukuliwa kuwa wataalamu wa afya watatumia sampuli ya damu kupima. Tunataka kujua watatumiaje? Kwa ufahamu wangu mdogo ugonjwa huu unapimwa kwa vidole,” alisema Nsimba.
Mkazi wa Kimara Abdallah Said aliipongeza kampeni hiyo, lakini alimsihi Makonda kabla ya kuianza, elimu ya kina kuhusu saratani ya tezi dume, itolewe kwa wanaume ili kujua madhara na namna ya kujikinga.
“Tunasikia sikia watu wakisema tezi dume… lakini baadhi hatujui inasababishwa na nini na madhara yake kwa wanaume. Ndio maana tunaomba elimu itolewe kwanza kabla ya kuanza kampeni.
“Tukielimishwa kampeni hii itakuwa msaada kubwa kwetu hasa kwa wale wenye kipato cha chini ambao wanashindwa kwenda hata hospitali kuangalia afya kwa maradhi mbalimbali yanayowasumbua,” alisema Said.
Lakini mtaalamu wa afya alitoa angalizo kuhusu kampeni hiyo.
Daktari wa Hospitali ya Bugando, George Kaanan alisema katika kampeni hiyo ni vyema wahusika wakakubali kwa hiari, kisha wakaelimishwa maana ya tezi dume kabla mchakato wa upimaji kuaanza.
Alifafanua kuwa upimaji wa ugonjwa huo ni wa kitaalamu zaidi na ili kupata majibu sahihi ni lazima kupimwa zaidi ya mara moja.
Mwananchi.
Comments