Kilichosababisha CHADEMA, CCM Wapewe Hati yenye Mashaka na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
amevishika pabaya vyama vikuu vya siasa nchini CCM na Chadema baada ya
kuhoji matumizi ya zaidi ya Sh19 bilioni.
Ripoti
hiyo ya ukaguzi wa hesabu iliyoishia Juni 30, 2017 iliyowasilishwa
bungeni wiki hii, inaonyesha kati ya vyama 19 vilivyopata usajili wa
kudumu, tisa havikuwasilisha taarifa za fedha wakati sheria inataka
viwasilishe ifikapo Septemba 30 kila mwaka.
Katika
ukaguzi huo, CAG anahoji matumizi ya zaidi ya Sh7 bilioni kwa Chadema
na zaidi ya Sh12 bilioni kwa CCM. CAG anasema katika ukaguzi walibaini
kuwa chama tawala kimeendelea kuwekeza katika kampuni nne na mikopo
yenye thamani ya Sh12 bilioni.
“Hata hivyo, tumejifunza kwamba mikopo hiyo haina faida yoyote iliyoonekana imeingia kwenye chama,” anasema CAG.
Pia
imebainika kuwa Sh80 milioni zilitambuliwa kama mapato ya uwekezaji
katika taarifa za fedha za CCM kutoka Jitegemee Trading Company Limited
lakini hazikuwa na kiambatanisho kinachothibitisha kama ni gawio au kitu
kingine.
CAG
anasema CCM bila kuanzisha sera, uwekezaji wa chama hicho upo katika
hatari ya kutumiwa vibaya na kwamba malengo yaliyowekwa yanaweza
yasifikiwe.
CAG
pia amebaini kupitia ukaguzi wa taarifa za fedha za CCM kwa mwaka
2016/2017 kuwa hazina taarifa za kutosha kuhusu mikataba, masharti,
kiasi na sababu za kutoa msaada wa Sh455.9 milioni kwa Radio Uhuru.
Taarifa
hiyo inaonyesha kuwa menejimenti ya CCM ilikopa na kuhamisha Sh337.1
milioni kutoka akaunti ya malipo ya pensheni kwenda akaunti ya katibu
mkuu wa chama na kupokewa kwa stakabadhi namba 156424.
Hata
hivyo, kiasi hicho hakijarejeshwa hadi wakati wa ukaguzi na kwamba,
matokeo yake ni uwezekano wa madai ya wafanyakazi wastaafu kutolipwa kwa
wakati.
CAG
anasema Aprili 11, 2015 Chadema iliingia makubaliano na mwanachama wake
ili awakopeshe Sh2 bilioni kwa ajili ya shughuli za chama.
Hata
hivyo, anasema hawakukuta nyaraka zinazoonyesha kiasi hicho cha mkopo
walichokubaliana iwapo kilitolewa na kupokewa na chama husika.
CAG
anasema katika ukaguzi, alikuta ankara ya kodi (tax invoice) yenye
namba 201508226 iliyotolewa Agosti 26, 2016 ya Sh866.6 milioni ambayo
ililipwa na mwanachama kwa niaba ya chama kwa ajili ya mabango ya
matangazo yaliyoletwa na mzabuni M/S Milestone International Co. Ltd.
Anasema
nje ya deni hilo, Sh715 milioni zililipwa kwa mwanachama kama marejesho
ya fedha iliyokopwa kulipia ununuzi wa mabango bila ya kuambatishwa
makubaliano ya kisheria.
Pia,
anahoji matumizi ya Sh2.3 bilioni ambazo ni makusanyo ya Chadema kwa
wanachama wake kwa mwaka 2014/15 na 2015/16, fedha ambazo zinadaiwa
kutopelekwa benki na matumizi yake kutotolewa kwa ajili ya ukaguzi.
Ripoti
ya CAG inaonyesha kuwa Chadema ilifanya ununuzi wa Sh2.1 bilioni bila
ushindani; malipo ya Sh240.1 milioni yenye nyaraka pungufu; na Sh558.9
milioni ambazo ni masurufu ambayo hayakurejeshwa.
Wakati
wa ukaguzi, CAG anasema alibaini vyama vinne vya Chadema (Kanda ya
Magharibi), NLD, Demokrasia Makini na ADC havina daftari la mali za
kudumu, hali inayosababisha ugumu wa kujua mali za chama, aina yake,
gharama na sehemu zilipo, hivyo kuziachia mali za chama kwenye hatari ya
kutumika vibaya.
“Kukosa
daftari la mali za kudumu ni kinyume cha Sheria ya Usajili wa Vyama vya
Siasa inayovitaka vyama vilivyosajiliwa kuwasilisha kwa msajili tamko
la mali zote kila mwaka” anasema CAG.
“Ninashauri
vyama vya siasa viwe na madaftari ya mali za kudumu ambayo yanahuishwa
mara kwa mara kutokana na ununuzi au mauzo ya mali,” inasema taarifa ya
CAG.
Kuhusu
malipo yenye nyaraka pungufu ya Sh735.978 milioni, CAG amebaini vyama
vitatu kati ya tisa vilivyokaguliwa, vina malipo yenye nyaraka pungufu
kinyume cha miongozo ya kiuhasibu pamoja na kanuni Na. 86 (1) na kanuni
na. 95 (4) ya Kanuni za fedha za Umma za mwaka 2001 ambazo zinaelekeza
kila malipo yawe yameambatanishwa na nyaraka sahihi.
Kutokana
na upungufu aliobaini, vyama vya CCM na Chadema vimepewa hati zenye
shaka huku Chama cha Wakulima (AFP), ADC, Demokrasia Makini, Chama cha
Kijamii, NLD, Sauti ya Umma na TLP vikipata hati mbaya.
chanzo:Mpekuzi.
Comments