Pia itajikita kuboresha shughuli nyingine katika mfumo wa mashtaka nchini.
Akiwasilisha mpango na makadirio ya bajeti ya wizara yake, Profesa Palamagamba Kabudi alisema bungeni jana kuwa watafuatilia na kutathmini matokeo yanayotokana na uendeshaji wa kesi za jinai.
Alisema shughuli nyingine ni kuweka mfumo wa kimkakati wa kusimamia masuala ya utajiri na rasilimali asilia; kuratibu mapitio ya mikataba na kubainisha maeneo yenye masharti hasi ili yarekebishwe.
Profesa Kabudi alisema wizara yake itapitia na kuboresha sheria ili ziendane na Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ahadi za Serikali.
Pia, alisema inaanza ujenzi wa majengo ya makao makuu ya Mahakama ya Tanzania mjini Dodoma ili kuhamishia rasmi shughuli zake makao makuu ya nchi kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Serikali.
Mbali ya ujenzi huo, alisema wizara itaendelea na ujenzi wa majengo ya mahakama nchini, yakiwamo mawili ya Mahakama Kuu yanayoendelea kujengwa katika mikoa ya Kigoma na Mara.
Alisema majengo mengine yatajengwa Morogoro, Mwanza, Dodoma na Singida.
Waziri huyo alisema pia kutafanyika ujenzi wa mahakama za wilaya 32 na za mwanzo 20.
Mali zataifishwa
Profesa Kabudi alisema Serikali imetaifisha mali kadhaa yakiwamo magari sita ya kifahari, kati ya hayo matano yakiwa aina ya Range Rover Vogue na Audi yaliyokamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba.
Alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara ilitaifisha mali zenye thamani ya Sh5.68 bilioni kutoka kwa washtakiwa waliotiwa hatiani.
Profesa Kabudi alisema fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya Sh908 milioni pia zilitaifishwa.
Mali nyingine ni fedha zilizotozwa kama faini Sh2.4 bilioni, pikipiki 34 zilizotaifishwa, mafuta, mashine za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa likitumika kusafirishia meno ya tembo.
“Katika kipindi hicho, mali za vyama vya ushirika vya Mwanza Nyanza Cooperative Union na Shinyanga (Shirecu) zikiwamo nyumba, viwanja na viwanda zilirejeshwa mikononi mwa Serikali kutoka kwa watu waliozichukua bila kufuata utaratibu wa kisheria,” alisema.
Profesa Kabudi alisema wizara ilipokea maombi 14 ya kurejesha watuhumiwa wa makosa ya jinai waliopo katika nchi za Rwanda, Zambia, Kenya, Malawi, Marekani na Uingereza.
“Wizara iliwasilisha maombi manne ya kurejeshwa nchini watuhumiwa wanaokabiliwa na makosa mbalimbali waliopo Rwanda, Uganda, Zambia na Afrika Kusini,” alisema.
Alisema makosa hayo yalihusisha ya usafirishaji wa dawa za kulevya, mauaji ya kimbari, wizi, mauaji, makosa ya kimtandao na ubakaji.
Waziri alisema kamati ya nidhamu ya mawakili ilipokea malalamiko 18 ya mawakili na kufanya jumla ya yaliyokuwa mbele ya kamati kufikia 48.
Comments