Siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita, yaani sawa na tarehe Tano Sha’ban mwaka 38 Hijiria, alizaliwa mjini Madina Imam Ali bin Hussein maarufu kwa jina la Imam Sajjad (as) mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw).
Imam Ali bin Hussein alipata elimu na maarifa huku akifikia akhlaqi na umaanawi kutoka kwa baba yake Imam Hussein (as), na vilevile kupata umashuhuri kwa uchaji-Mungu na ibada kati ya watu wa zama zake.
Ni kutokana na kusujudu kwake kwingi ndipo akatokea kuitwa ‘Sajjad’ yaani mtu anayesujudu sana. Imam Ali bin Hussein alishuhudia tukio la Ashura Karbala ambapo watu wa familia ya Mtume akiwemo baba yake Imam Hussein waliuawa shahidi, hata hivyo kutokana na ugonjwa, hakuweza kushiriki katika jihadi.
Baada ya tukio hilo, mtukufu huyo kwa kushirikiana na shangazi yake, Bibi Zainab (as), walifichua dhulma za watawala wa Bani Umayyah kwa watu. Aidha Imam Sajjad alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu hadi alipofariki dunia mwaka 94 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 1126 iliyopita alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo.
Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa.
Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.
Siku kama ya leo miaka 294 iliyopita, alizaliwa mjini Königsberg, Ujerumani na katika familia ya kati Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa nchi hiyo.
Baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya hisabati, theolojia na falsafa Kant alijishughulisha na kazi ya ufundishaji vijijini. Baadaye na akiwa na umri wa miaka 46 msomi huyo alifanikiwa kuwa muhadhiri wa falsafa katika chuo kikuu cha mji alikozaliwa wa Königsberg. Katika miaka yote ya utafiti wake na kufundisha falsafa, alipata kuandika vitabu tofauti ambavyo baadhi vipo katika maktaba kubwa duniani.
Kadhalika mwanafalsafa huyo mkubwa alifanikiwa kuasisi mfumo wa kifikra maalumu katika uga huo. Kwa imani ya Immanuel Kant, ndani ya mwanadamu kuna hisia maalumu ya kitabia ambayo huweza kutoa hukumu kwamba kitendo hiki ni chema na kile ni kiovu.
Hii ikiwa na maana kwamba, mwanadamu binafasi anaweza kutenda mema na maovu, lakini ile hisia yake ya kitabia ndio huweza kumueleza kwamba kitendo fulani ni chema au kibaya na kwamba lau kama si kuwepo kwa hisia hiyo, basi mwanadamu asingeweza mwenyewe kujilaumu baada ya kutenda jambo fulani.
Immanuel Kant alifariki dunia tarehe 12 Februari 1904 mjini Königsberg akiwa na umri wa miaka 80 huku akiwa ameishi maisha yake yote akiwa kapera (yaani bila kuoa.)
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania.
Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao.
Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania. Manowari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani.
Miaka 114 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer.
Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia.
Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel.
Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje.
Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapigano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui.
Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo wake mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.
Hii nikwahisani ya parstoday.
Comments