Ijumaa tarehe 6 Aprili 2018.

Ijumaa tarehe 6 Aprili 2018Leo ni Ijumaa tarehe 19 Rajab 1439 Hijria sawa na Aprili 6, 2018.

Tarehe 19 Rajab miaka 1430 iliyopita vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. 
Vita vya Tabuk vilikuwa miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw). 
Sababu ya kuelekea kwenye vita hivyo ni kwamba msafara wa kibiashara wa Sham ulimpasha habari Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba Mfalme wa Roma ametayarisha jeshi kubwa na kuanza safari ya kuelekea Madina. 
Kwa msingi huo Mtume (saw) aliwaamuru Waislamu wajitayarisha kwa ajili ya vita. 
Waislamu wengi waliitikia wito huo licha ya masafa marefu ya kuelekea Tabuk, mashaka ya safari hiyo, jua kali na kuwadia kwa kipindi cha mavuno. Hatimaye jeshi la wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili katika medani ya vita lakini halikukuta jeshi la Roma eneo hilo. 
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, moyo wa kusabilia roho zao kwa ajili ya dini na utayarifu wao kwa ajili ya kukabiliana na adui. 
Vita hivyo pia vinajulikana katika historia kwa jina la al Fadhiha kwa maana ya mfedheheshaji kwa sababu viliwafedhehesha baadhi ya wanafiki katika safu za Waislamu. 
Miaka 438 iliyopita na katika siku kama ya leo, ardhi ya Ureno moja kati ya nchi iliyokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16 iliunganishwa na Uhispania. 
Ureno ilikuwa ikihesabiwa kama mpinzani mkuu wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. 
Hata hivyo pole pole Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile kufuatia hali mbaya ya kiuchumi. 
Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. 
Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa nchi hiyo.
Siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita Jaafar Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. 
Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. 
Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani. 
Na tarehe 6 Aprili katika siku kama hii ya leo miaka 24 iliyopita Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. 
Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994. 
 Hii nikwahisani ya parstoday.

Comments