Dk. Shein: Mzee Karume ana heshima ya pekee.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema azma ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuandaa kongamano la kumbukumbu ya kumuenzi marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ni ya kupongezwa kutokana na kutambua juhudi za kiongozi huyo aliyewapigania wanyonge.

Aliyasema hayo jana alipokutana na Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Prof. Mark Mwandosiya, Ikulu mjini Zanzibar.

Alisema marehemu mzee Karume ana heshima ya pekee kwa Zanzibar na Tanzania nzima, uamuzi wa chuo hicho kuandaa kongamano hilo ni hatua moja wapo ya kumuenzi  na kumthamini muasisi huyo.

Aliongeza kuwa mzee Karume alikuwa na dira na ndio maana alifanya mambo mengi makubwa ambayo yataendelea kukumbukwa kutokana na umuhimu wake.

Alieleza kuwa mzee Karume ndie aliesimamia mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yaliwakomboa Wazanzibari na kuwatoa katika unyonge na hatimae kuondosha ubaguzi wa aina zote.

Aidha, alieleza kuwa kufanyika kwa mapinduzi ni jitihada za mzee Karume na viongozi wenzake ambapo jitihada hizo zinafaa kuenziwa pamoja na kutunzwa na kudumishwa ili na vizazi vijavyo viweze kuzifahamu.

Alisema kuwa kuna kila sababu ya kutoa pongezi kwa chuo hicho kwa kwa hatua hiyo ya kutambua mchango mkubwa wa marehemu Karume ambaye pia, ni muasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hatimae kuundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa marehemu mzee Karume na marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere waliziunganisha Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 na hadi hivi leo muungano huo umejijengea sifa kubwa ndani na nje ya Afrika na kuwa wenye manufaa makubwa kwa Watanzania wote.

Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuiimarisha kampasi yake ya Zanzibar ambayo hivi sasa inasomesha kada mbali mbali sambamba na kuongezeka kwa wanafunzi na kusisitiza kuwa hiyo yote inatokana na uongozi thabiti uliopo katika chuo hicho.

Chanzo:zanzibarleo.

Comments