Leo
Jumapili Aprili 15, 2018 Chama cha ACT Wazalendo kimetoa tathmini na
uchambuzi wake juu ya ripoti mpya ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.
==>Soma
taarifa hiyo iliyotolewa leo Aprili 15, 2018 na Kiongozi wa ACT
Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe.
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, Prof. Mussa Assad ametoa
taarifa yake ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka
2016/17. Kwa sasa taarifa hiyo iko wazi kwa umma, baada ya kuwa
imekabidhiwa rasmi bungeni. Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na
kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza
wajibu wetu wa kuisimamia Serikali, kama chama cha Upinzani bungeni.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu Magufuli tayari amechukua
hatua za kiuwajibikaji dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa zenye hati isiyoridhisha, hatua hii ni ya njema, ACT
Wazalendo tunampongeza kwa jambo hilo. Hata hivyo, baada ya kuipitia
ripoti husika, tumegundua kuwa CAG ameibua masuala mazito ambayo yana
madhara makubwa kwenye mfumo mzima wa Bajeti ya Nchi kama
hayatashughulikiwa. Tumewaita hapa kuyazungumzia hayo.
Maeneo 8 ya Hatari Katika Ripoti ya CAG.
1.
Mawaziri Wanavunja Sheria ya Ukaguzi. Tunaomba kutoa angalizo na
muongozo wa kisheria juu ya hadaa inayofanywa na Serikali juu ya
kinachoitwa “Majibu ya Mawaziri juu ya Ripoti ya CAG”. Kisheria Mikutano
hii ya Mawaziri na wanahabari inayoendelea ni kinyume na Sheria ya
Ukaguzi ya Umma, kifungu cha 38(1) na (2), ambacho kinaelekeza waziwazi
kuwa Maafisa Masuuli ndio wanapaswa kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa
na CAG, tena majibu husika hupaswa kuletwa mbele ya Kamati za Bunge za
PAC na LAAC. Kwa utaratibu wa kawaida wa kiwizara, maafisa masuuli ni
Makatibu Wakuu wa Wizara na si Mawaziri.
2.
6% ya Fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilizokwenda.
Katika ukaguzi wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni Bajeti ya kwanza ya
Serikali ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kuwa kati ya Bajeti ya
shilingi 29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza
kukusanya shilingi 25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo
visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na
washirika wa maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi
4.2 trilioni, sawa na 15% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Jambo la
kushtusha na linalohitaji majibu ya Serikali ni kwamba, CAG amegundua
kuwa katika fedha zote zilizokusanywa, shilingi 25.3 trilioni, ni
shilingi 23.8 trilioni tu ndio zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya
watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni
yatokanayo na amana za serikali na riba, shilingi 1.5 trilioni
zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi. Fedha hii ambayo matumizi yake
hayajulikani ni sawa na 6% ya Fedha zote zilizokusanywa mwaka huo.
Matrilioni haya ambayo Serikali imeyapoteza ni zaidi ya mara mbili ya
Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka husika (672 bilioni).
3.
Bajeti ya Tanzania haina Hadhi (Credibility) tena. Taarifa ya CAG
inaonyesha kuwa Bajeti inayopitishwa na Bunge haina Hadhi (Credibility)
tena, kwani kuna matumizi makubwa ya nje ya Bajeti kinyume na
ilivyoidhinishwa na Bunge. Kwa mfano, CAG ameonyesha kuwa Bunge lilitoa
Kibali kwa Serikali kukopa mikopo ya ndani yenye thamani ya TZS 5.4
trilioni lakini Serikali ilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa kwa
10%, ambapo zilikopwa shilingi 5.9 trilioni, yaani bilioni 500 zaidi ya
ukomo wa kukopa uliotolewa na Bunge. Haya ni matusi makubwa kwa Bunge,
yanaondoa hadhi ya bajeti inayopotishwa na Bunge.
4.
Heshima na Hadhi ya Bunge letu vinaondolewa. Kazi Kuu ya Bunge ni
kuidhinisha Bajeti inayoletwa bungeni na Serikali, mara baada ya
mjadala. Kwa sasa heshima na hadhi ya Bunge vinaondolewa kutokana na
Bajeti iliyopitishwa kutokutekelezwa, hasa kwa kiasi cha fedha
zilizoidhinishwa na bunge kwaajili ya miradi ya Maendeleo kutokutolewa.
Taarifa ya CAG imeonyesha kuwa, kwa ujumla, ni 68% tu ya Bajeti ya
Maendeleo ndio ilitekelezwa, hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Serikali
za Mitaa, ambapo ni 51% tu ndiyo ilitekelezwa.
5.
Mabilioni ya Fedha za Watanzania yametumika kulipa Madeni ambayo
hayakuidhinishwa na Bunge. Taarifa ya CAG imeonyesha pia kuwa Serikali
ilitumia zaidi ya shilingi 219 bilioni, kulipa madeni ya nyuma. Lakini
matumizi hayo hayakuwa sehemu ya Bajeti iliyoletwa na Serikali na
kuidhinishwa na Bunge. Hivyo madeni hayo ni hewa, na ulipwaji wake ni
matumizi nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge.
6.
TRA Wametoa Takwimu za Uongo za Mapato ya Kodi ya zaidi ya shilingi 2.2
trilioni. Taarifa ya CAG imeonyesha, kwa mwaka wa fedha wa 2016/17,
Mamlaka ya Mapato nchini, TRA ilituhadaa kwa kutangaza kuwa imekusanya
fedha zaidi kuliko uhalisia wake. Kati ya kiasi cha shilingi 15.1
trilioni ambazo TRA ilitutangazia kuwa imezikusanya kwa mwaka 2016/17,
shilingi 2.2 trilioni hazikuwa za TRA. Kimsingi fedha hizo si makusanyo
ya kodi, bali TRA walizikusanya tu kama wakala wa asasi, taasisi na
wakala nyengine za Serikali. Makusanyo halisi ya fedha za kodi yalikuwa
ni shilingi 12.9 trilioni tu. Uongo huu wa TRA kutangaza hata mapato
yasiyo yake umepelekea kutokea kwa shilingi 325 bilioni ambazo
zilihesabiwa mara mbili (double accounting) kwenye Hesabu Jumuifu za
Taifa, na hivyo kuchafua hesabu za Taifa na kuondoa uhalali wake
kitakwimu. Pia taarifa ya CAG imeonyesha kuwa TRA hudanganya makusanyo
wanayotangaza kila miezi mitatu.
7.
Serikali kwa ujumla imepata Hati Chafu. Taarifa ya CAG ya Ukaguzi wa
kwanza wa makusanyo na matumizi ya kibajeti ya Serikali ya awamu ya
tano, imeonyesha kuwa, kwa ujumla, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
imepata Hati Chafu, kwa kuwa Hesabu Jumuifu za Taifa (consolidated
accounts) zimepata Hati ISIYORIDHISHA (Chafu). Sababu za kutolewa Hati
hii kwenye taarifa ya CAG ni pamoja na fedha kutumika kinyume na mafungu
yaliyopangwa na Serikali yenyewe, kupotea kwa shilingi 1.5 trilioni,
TRA kutangaza mapato ambayo si yake kuwa ni yake na hivyo kupelekea
‘double accounting‘ (kuhesabiwa mara mbili kwa fedha) kwenye mapato.
Hesabu Jumuifu za Taifa ndio Hazina ya Taifa, kupata Hati Chafu ni
hatari sana kwa mustakabali wa Taifa.
8.
CAG hajakagua Ununuzi wa Ndege. Licha ya kuwa taarifa hii ya CAG ni
taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo kadhaa ambayo CAG
ameyaacha, ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL
ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17.
Mapendekezo: Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo hayo 8, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:
1.
Tunawaomba Wenyeviti wa Kamati za Bunge za PAC na LAAC kufikisha suala
Mawaziri kuzungumza kwenye vyombo vya habari kujibu ripoti ya CAG kwa
Spika wa Bunge, ili Spika amjulishe Waziri Mkuu juu uvunjifu huu wa
sheria unaofanywa na Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano, wakiwemo
Mawaziri wazoefu wa taratibu za kibunge kama Waziri William Lukuvi na
Waziri Harrison Mwakyembe. Mawaziri hawa wanafanya ‘spinning’ (hadaa)
ili kuficha madudu ambayo CAG ameyaibua. Tunawaasa waache jambo hili, na
wafuate sheria.
2.
Tunaisihi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kuomba kibali cha
kukutana haraka na kuagiza Ukaguzi Maalumu wa shilingi 1.5 trilioni
ambazo zimepotea na Serikali ya Awamu ya Tano imeshindwa kuzitolea
maelezo kutoka kwenye makusanyo ya mwaka 2016/17. Hii ni mara ya kwanza
kwenye historia ya nchi yetu kwa Serikali kukusanya fedha, kutozigawa
kwenye Wizara, Idara, Wakala na Mikoa, kutoonekana matumizi yake na CAG
kushindwa kuzikagua. PAC itimize wajibu wake haraka iwezekavyo. Wakati
huu ukaguzi huu unafanyika, kama ilivyofanyika kwa Wakurugenzi wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa waliopata Hati Isiyoridhisha, Rais
amsimamishe kazi Katibu Mkuu Hazina na Mlipaji Mkuu wa Serikali, kwa
kushindwa kusimamia vema Fedha za Umma na kupelekea Hesabu Jumuifu za
Taifa (consolidated accounts ) kupata Hati isiyoridhisha ili kupisha
uchunguzi huu.
3.
Tunalishauri Bunge litake maelezo ya kina ya Serikali kuhusu kukopa
bilioni 500 zaidi ya Serikali yenyewe ilivyoomba na kuidhinishiwa na
Bunge. Ni matarajio yetu kuwa Bunge litachukua hatua dhidi ya Serikali
kwa kukiuka Sheria ya Bajeti ambayo inakataza kabisa Serikali kukopa
zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge. CAG ameonya katika Taarifa
yake kwa kusema yafuatayo kuhusu jambo hili “sehemu kubwa ya mtaji wa
mabenki unakuwa umefungwa kwenye fedha walizokopesha serikali kwa muda
mfupi na muda mrefu; na matokeo yake, riba ya kukopesha kwa watu binafsi
inakuwa kubwa na gharama za maisha zinakuwa juu”. Ukopaji wa namna hii
unafanya UCHUMI KUSINYAA kwani unaondoa fedha kwenye mzunguko na
kushusha uzalishaji.
4.
Tunalishauri Bunge liiwajibishe Serikali kwa kutoheshimu Bajeti ambayo
Bunge lilipitisha. Bunge linapaswa kulinda hadhi na heshima yake kwa
kuhakikisha fedha za maendeleo linazozipitisha zinapelekwa kama
ilivyopangwa. Bunge lisipofanya hivyo litaendelea kudharaulika. Spika wa
Bunge asimame imara kulinda Mhimili wa Bunge dhidi ya uvunjifu wa
sheria wa Serikali kwenye masuala ya Fedha za Umma, hasa wakati huu
ambao CAG ameonyesha Fedha nyingi zimetumika kinyume na utaratibu huku
fedha za maendeleo zilipitishwa na Bunge zikiwa hazipelekwi.
5.
Ni imani yetu kuwa Bunge litawawajibisha wote waliohusika katika malipo
ya madeni ambayo hayakuidhinishwa na Bunge letu. Madeni haya pia
yanapaswa kujulikana ni yepi kwani CAG anaonyesha kuwa Wizara ya Ujenzi
ndiyo imelipa zaidi madeni ya namna hii ambayo hayakuwa kwenye bajeti.
Utaratibu wa namna hii ukiachwa bila kuchukua hatua, utatoa mwanya wa
fedha za umma kupotea tu bila maelezo yoyote.
6.TRA
kwa makusudi, na kwa lengo la kufanya hadaa walitangaza kiwango kikubwa
zaidi cha makusanyo kuliko kiwango ilichopaswa kutangaza kuwa
imekusanya. Tunatarajia kuwa Bunge litaitaka TRA iombe radhi Watanzania
kwa upotoshaji huo ilioufanya na kutaka wote waliohusika kwenye hadaa
hii wawajibike. Pia tunawasihi TRA kuzingatia weledi wa kazi yao kwa
kutangaza makusanyo yao tu, na kuacha fedha za taasisi na asasi nyengine
kama VETA, TPA, Bodi ya Mikopo nk (ambazo TRA huzikusanya kama Wakala
wa taasisi hizo) zitangazwe na wahusika wenyewe.
7.
Tunaishari Serikali kurejesha utaratibu wa kupanga matumizi ya kila
mwezi ya fedha za umma kwa Hazina, na kuacha utaratibu wa sasa wa Ikulu
kupanga matumizi ya kila mwezi. Utaratibu huu wa sasa unamuexpose
(unamweka kwenye mazingira hatari) Rais, hasa kutuhumiwa kwa ufisadi na
kukiuka sheria iwapo kuna makosa ya upotevu wa fedha kama haya ambayo
CAG ameyaibua katika taarifa yake na kupelekea hesabu jumuishi za
Serikali kupewa Hati Chafu. Tunashauri pia kuachwa kwa mfumo wa Rais
wetu kutamka kugawa Fedha kinyume kabisa na Bajeti iliyopitishwa na
Bunge.
8.
Ni matarajio yetu kuwa katika ripoti ya mwakani ya CAG, Taifa litapata
wasaa wa kuona ukaguzi wa ununuzi wa ndege za shirika la ndege la Taifa,
ATCL na ukaguzi wa manunuzi ya kandarasi ya ujenzi wa kiwanja cha ndege
cha Chato. Ni muhimu sana kwa CAG kuona mambo yanayosemwa na umma na
kuchukua hatua za ukaguzi kwani yeye ndiye mlinzi wa fedha za umma.
Hitimisho
ACT
Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao kutekeleza
wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge tusipotekeleza wajibu wake
nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu ya nje ya Bajeti na ya kinyume
cha sheria. Ni dhahiri, kwa dalili hizi zilizoonyeshwa na taarifa ya
CAG, kuwa Wabunge tusipoisimamia na kuidhibiti Serikali ya awamu ya
tano, Nchi itafilisika kutokana na maamuzi ya hovyo, yasiyo ya kibajeti,
yanayoenda kinyume na kanuni za kifedha na kiuchumi, na yasiyozingatia
sheria za Nchi yetu.
Sisi
ACT Wazalendo tutaendelea kuichambua taarifa hii ili kuibua masuala
zaidi. Haya tuliyoyaeleza leo ni machache sana, hatujagusia kabisa
mapungufu kwenye deni la Taifa, kulinganisha na mambo mengi ambayo CAG
ameeleza. Tunawahimiza Wabunge na Wananchi kwa ujumla kusoma taarifa ya
CAG kwa ukamilifu. Taarifa ya mwaka huu ina hoja nzito kuliko wakati
mwingine wowote ule. Haijawahi kupata kutokea Serikali ya Nchi
kulidgarau Bunge letu kama ilivyo kwa kiwango kilichoonyeshwa na taarifa
ya mwaka huu ya CAG.
chanzo:mpekuzi.
Comments