VIONGOZI na watendaji wa majimbo wa mkoa magharibi, wametakiwa
kufanya kazi kwa pamoja ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiutendaji
katika kukiimarisha chama chao.
Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Mohammed Rajab Soud, aliyasema hayo
katika mkutano wa tathmini kwa ziara yake aliyoifanya hivi karibuni
katika majimbo ya mkoa huo kwa ajili ya kukutana na wanachama na
viongozi wa chama hicho uliofanyika tawi la CCM Kiembesamaki.
Alisema, umoja, mashirikiano na uzalendo kwa viongozi na wanachama wa
chama hicho ndio njia pekee itakayoweza kukimarisha chama na kuendelea
kukipatia ushindi.
Aidha, alisema wakati umefika kwa viongozi na watendaji wote wa chama
kuachana na fitna, chuki na makundi badala yake wafanye kazi kwa pamoja
katika kusimamia na kutekeleza ilani ya chama hicho.
Akizungumzia ahadi zilizotolewa na viongozi wa majimbo, alisema ni
jambo la msingi kuhakikisha wanatimiza ahadi hizo kwa haraka ili chama
hicho kiendelee kupewa ridhaa na wananchi ya kuendelea kushika dola.
Hata hivyo, alisema uongozi wa mkoa huo umekusudia kuleta mabadiliko
makubwa katika kusimamia na kutekeleza ilani ya chama kwa asilimia 100
na kuona wananchi wanapata maendeleo kupitia mambo mbalimbali ikiwemo
afya, elimu, miundombinu ya barabara na mambo mengine.
Mjumbe wa Kamati ya siasa ya mkoa, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema
CCM tokea enzi za TANU na ASP haiyumbishwi kwani viongozi wake madhubuti
kutokana na kuongoza kwa kufuata maadili, katiba na kanuni za chama
chao.
Alisema, hivi sasa kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuleta
mabadiliko ndani ya chama chao kupitia ilani ambayo Makamu Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ameitekeleza kwa asilimia kubwa.
Hivyo, aliwasisitiza viongozi hao kushirikiana na wanachama na
wananchi wapenda amani na maendeleo kuhakikisha CCM inaendelea kushika
dola Zanzibar na Tanzania bara.
Ayoub, ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, akitoa
ufafanuzi kuhusu vifaa vya usafi unaotekelezwa na mabaraza ya vijana,
alisema mpango huo upo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wake
ambapo kwa sasa manispaa yanamalizia kuimarisha kanuni.
Kwa upande wao viongozi wa majimbo, walisema ziara ya Mwenyekiti huyo
imewaleta pamoja na kubaini kasoro mbali mbali ziliomo majimboni mwao
na kuahidi kuzifanyia kazi kwa haraka.
chanzo: zanzibarleo.
Comments