Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani iliyoadhimishwa kote duniani hapo jana imeeleza kwamba, endapo mwenendo huu wa uhaba wa maji safi na salama ya kunywa utaendelea, basi hadi kufikia mwaka 2030 takribani watu bilioni mbili duniani watalazimika kutumia maji ya kunywa yasiyo safi na salama.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, takribani watu milioni 700 watalazimika kuwa wakimbizi kufikia mwaka 2030 kutokana na uhaba wa maji safi na salama ya kunywa katika maeneo yao.
Akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Maji Duniani, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, "hadi sasa kihistoria maji yamethibitika kuwa ni chachu kwa ajili ya ushirikiano na sio kwa ajili ya migogoro.
Lakini bila udhibiti maalumu wa rasilimali zetu za maji tunahatarisha kuongeza migongano baina ya jamii na sekta na hata kuongeza mivutano miongoni mwa nchi.”
Kushadidi kwa ukame na kutonyesha mvua kwa wakati ni baadhi ya sababu zinazotajwa kuwa zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotaabika kwa kukosa maji safi na salama ya kunywa.
Nchi zinazokabiliwa na vita na machafuko kama Yemen, kaskazini mwa Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Myanmar zinatajwa kuwa zinakabiliwa zaidi na hatari ya kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama ya kunywa.
chanzo:parstoday..
Comments