Ulinzi waimarishwa mahakamani kesi ya viongozi wa Chadema.

chademaJeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeimarisha ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kudhibiti umati wa watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokusanyika nje ya mahakama, wasiingie kusikiliza kesi inayowakabili mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na viongozi wenzake watano.

Mbowe na wenzake wameshafikishwa mahakamani hapo wakitokea mahabusu ya Segerea wakikabiliwa na mashtaka nane yakiwemo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline, Februari 16, mwaka huu, uasi na kuhamasisha chuki.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho (Zanzibar) Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chama hicho Vicent Mashinji na wengine.

Baadhi ya wabunge wa Chadema, wafuasi wa chama hicho na wananchi wengine waliofika mahakamani kufuatilia kesi hiyo ni  Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Abdallah Safari, Mbunge Joseph Haule ‘Prof. Jay.

Comments