KAIMU Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' amesema kwa nguvu waliyonayo sasa wana uwezo wa kuifunga Yanga kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara na kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.
Simba iliondoshwa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika na Al Masry ya mjini hapa kwa faida ya bao la ugenini, baada ya matokeo ya suluhu kwenye mechi ya marudiano wakati mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Try Again alisema baada ya kuenguliwa kwenye michuano hiyo wamerejesha nguvu zote Ligi Kuu na wana imani ubingwa umewakalia kwenye njia yao.
"Kwa namna tulivyojipanga kama uongozi, nafasi ya kutwaa ubingwa tunayo. Timu inacheza vizuri na kwa nidhamu kubwa.
"Tumefurahishwa na kiwango cha timu kwenye mechi ya marudiano. Kama siyo mapungufu machache ya mwamuzi tulikuwa na uwezo wa kushinda. Wachezaji walijituma na walicheza vizuri.
"Kama tutakwenda kwa morali hii tuna uwezo wa kuifunga Yanga kwenye mchezo ujao na tukaendelea kusalia kileleni mpaka tutakapotwaa ubingwa, tuna imani kubwa na timu yetu," alisema Tryagain, ambaye alikuwa imara kudhibiti fitna za Waarabu kwenye mchezo huo wa marudiano mjini hapa.
Comments