Jeshi
la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia watu saba kwa matukio mbalimbali
ya uhalifu, wakiwamo vijana watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya
mlinzi wa SUMA-JKT.
Wanadaiwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumpora bunduki na kutokomea nayo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema Februari 26, mwaka
huu ya saa 1:30 jioni, vijana hao wakiwa na mapanga, walimvamia na
kumshambulia mlinzi huyo, Chewe Wilson (34), akilinda kituo cha mafuta
cha Manyanya kilichopo Uyole.
Aliwataja
vijana hao ni Hamis Shaban (19) na Ibrahim Mbilinyi (22) wote wakazi wa
Itezi, Stan Wema (21) mkazi wa Uyole, Bahati Laulend (22) mkazi wa
Iduda na Sambaa Samson (32) mkazi wa Isyeseye.
Alisema
vijana hao baada ya kumjeruhi wakidhani amekufa walimpora bunduki aina
ya Shortgun, mali ya SUMA-JKT aliyokuwa anaitumia na kutokomea nayo.
Hata
hivyo, alisema mlinzi huyo alikutwa na wasamaria wema akiwa hai na
kukimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya, lakini
akafariki kesho yake kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Kufuatia
tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa
kuwakamata vijana hao na baada ya kupekuliwa walikutwa na bunduki hiyo
waliyopora yenye namba za usajili 009009906-MP-18EM-M wakiwa wameificha
nyumbani,” alisema Mpinga na kuongeza:
“Vilevile
vijana hao wanaojiita ‘Doshaz’ walikutwa na mapanga matatu ambayo
mojawapo lilitumika kumjeruhi Chewe na maganda matatu matupu ya risasi,
tulipowahoji walikiri kuhusika na tukio hilo na tunatarajia kuwafikisha
mahakamani upelelezi ukikamilika.”
Aliongeza kuwa vijana hao walieleza kuna mtu aliwatuma ili wakaibe bunduki hiyo kwa ahadi ya kupewa zawadi ya Sh. milioni tatu.
Katika
tukio lingine, watu wawili akiwamo mzee wa miaka 60, wanashikiliwa na
jeshi hilo kwa kosa la kutengeneza bunduki ya kienyeji aina ya Shortgun
pamoja na kukutwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea silaha
hiyo.
Mpinga aliwataja ni Mzee Fadhili Mayenga (60) na Mashaka Samuel (38), wote wakazi wa Kijiji cha Kambikatoto Wilaya ya Chunya.
Alisema
watuhumiwa hao walikamatwa Machi Jumamosi mchana kufuatia msako mkali
uliofanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kwa
mujibu wa Mpinga, baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa na vifaa
mbalimbali vinavyotumika kutengeneza silaha hiyo pamoja na risasi 25 za
kienyeji ambazo hutumika kwenye silaha hiyo.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokuwa umekamilika.
chanzo:Mpekuzi.
Comments