Mshitakiwa
wa Kesi ya uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, James
Rugemalira amewasilisha maombi matatu katika Mahakama ya Rufaa ikiwemo
ombi la kusudio la kukata rufaa kupinga kunyimwa dhamana na Mahakama Kuu
Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’.
Ombi
lingine ni la kuitaka Mahakama hiyo kumuingiza katika maombi hayo,
Mtuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, Habinder Sethi ambapo Rugemalira
ameiomba Mahakama imuingize Sethi kama mtu muhimu katika kesi hiyo.
Maombi
hayo yamewasilishwa jana Machi 5, 2018 mahakamani hapo na Rugemalira
mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa
Benard Luanda na Jaji Gerald Ndika.
Hata
hivyo, kulikuwa na mvutano kati ya upande wa Jamhuri na upande wa
mshtakiwa baada ya Jamhuri kuweka pingamizi kwa kuiomba Mahakama ya
Rufaa kuyatupilia mbali maombi hayo kwa madai kuwa, muwasilishaji
alitumia kanuni zisizo sahihi huku upande wa utetezi ukipinga pingamizi
hilo kwa madai kwamba Jamhuri haikuwasilisha pingamizi hilo kwa
maandishi.
Kufuatia mvutano huo, Jaji Luanda amesema wanaahirisha maombi hayo na watapanga tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi.
chanzo:Mpekuzi.
Comments