Seikali ya Baghdad imesisitiza mara nyingi kwamba kundi hilo la Hash'd as-Sha'bi la Iraq ni sehemu isiyotenganishika na vyombo vya usalama vya Iraq na kwamba likiwa ni kundi rasmi linalofuata amri za kamandi kuu ya majeshi ya Iraq, tayari limetambuliwa rasmi na bunge la nchi hiyo.
Hashd as-Sha'abi ilikuwa na nafasi muhimu sana katika kulitokomeza kundi la kigaidi la Daesh ambalo lilikuwa likitishia usalama wa Iraq na eneo zima la Mashariki ya Kati.
Kuhusu suala hilo, Mkuu wa Kituo cha Sera za Kiarabu mjini Geneva amefichua nafasi hasi ya watawala wa Abu Dhabi katika kuzua vurugu na kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati.
Akibainisha zaidi, Sami al-Jaluli, mwandishi wa Kitunisia ambaye pia ni mkuu wa kituo kilichotajwa amesema kuwa serikali ya Imarati inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuanzisha migogoro na kuendesha vita vya kimadhehebu na kikabila katika eneo.
Amesema kwa sasa watawala wa serikali hiyo wanashirikiana kwa karibu na wenzao wa Saudia katika kueneza migogoro na vita hivyo katika eneo.
Imarati na watawala wengine wa Kiarabu wanaounga mkono ugaidi wanatambua vyema kwamba uwepo wa Hashd as-Sha'abi nchini Iraq unaashiria wazi kumalizika kwa kipindi cha makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayoungwa mkono na watawala hao.
Kwa msingi huo na katika duru hii mpya ya uingiliaji wa watawala wa Kiarabu nchini Iraq, maafisa wa Imarati wameanzisha uchochezi wa kuandaa mazingira ya kuvunjiliwa mbali kundi la wapiganaji wa kujitolea wa Iraq, yaani Hashd as-Sha'abi.
Hii ni katika hali ambayo bunge la Iraq tarehe 26 Novemba 2016 lilipitisha rasmi na kwa wingi wa kura mswada wa kuunganisha kundi hilo la wapiganaji wa kujitolea na jeshi la taifa.
Kundi la Hashd as-Sha'bi ambalo linaundwa na makundi na makabila tofauti ya Iraq lilibuniwa kufuatia pendekezo la Ayatullah Sistani, marja' na mwanazuoni mashuhuri wa Iraq kufuatia kutekwa na magaidi wa Daesh mji wa Mosul tarehe 10 Juni 2014.
Sisitizo la viongozi wa Iraq la kuendelea shughuli za Hashd as-Shaabi ni jibu tosha kwa mashinikizo ya serikali za Magharibi na watawala wa Kiarabu na hasa Saudi Arabia na Imarati ambao kwa mbinu tofauti wanaishinikiza serikali ya Iraq ifutilie mbali kundi hilo la wapiganaji wa kujitolea.
Serikali za nchi za Magharibi na watawala wa Kiarabu wamefikisha uingiliaji wao huo wa mambo ya ndani ya Iraq katika kiwango cha kushurutisha, kwa njia isiyo ya moja kwa moja, msaada wao wa kiuchumi kwa ujenzi mpya wa Iraq baada ya kutokomezwa magaidi wa Desh, na suala la serikali ya Baghdad kuchukua hatua ya kulifutilia mbali kundi la Hashd as-Sha'abi na pia kujitenga na nchi zilizo mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya ugaidi, zikiwemo Iran na Syria.
Iraq baada ya kuangamizwa magaidi wa Daesh inakabiliwa na njama tofauti za nchi za Magharibi na washirika wao wa kieneo pamoja na makundi ya kigaidi wanayoyaunga mkono.
Hali kama hiyo bila shaka inatoa udharura wa viongozi wa Iraq kuwa makini na waangalifu zaidi mbele ya siasa na misimamo ya uingiliaji ya nchi za Magharibi na watawala vibaraka wa nchi za Kiarabu, ikiwemo Imarati.
chanzo:parstoday.
Comments