
Akitoa Mafunzo kwa Viongozi hao wa Serikali za Mitaa Afisa Elimu kwa Umma kutoka Zaeca Sheha Kombo Hamad amesema kuna baadhi ya viongozi hao wanatumia vibaya madaraka yao ya uongozi waliyopewa kwa kujimilikisha mali za umma kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo ni kosa kisheria.
Amesema ili kiongozi awe muadilifu katika kusimamia mali za umma nivyema kukwepa aina zote za vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi pamoja na kuwacha tama anaposimamia mali za serikali zilizopo.
Kombo amesema hivi sasa Serikali kwa kushirikiana na Zaeca inampango mkakati katika kudhibiti viashiria pamoja na mianya yote ya rushwa katika ngazi mbalimbali kwa kuanzia na serikali kuu hadi serikali za mitaa ili kuwaondoshea malalamiko wananchi wanaonyimwa haki zao za msingi.
Aidha amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa katika kudhibiti vitendo hivyo ni pamoja na kupitishwa kwa sheria za usimamizi wa fedha,sheria ya kodi,Kuboresha mfumo wa utumishi wa umma pamoja na kupitisha kwa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ili iwe rahisi katika kuwachukulia hatua za kisheria wanaobainika na vitendo hivyo vinavyodumaza maendeleo nchini.
Kwaupande wao Madiwani na Masheha waliopatiwa mafunzo ya Rushwa na Uhujumu uchumi wamesema wameipokea vyema elimu hiyo waliyopatiwa na mamlaka hiyo na kuahidi kuifanyia kazi na kujiepusha na mdudu rushwa anaedumaza maendeleo.
Wakati huo huo wameitaka Zaeca kufanya uchunguzi wa kina kila taasisi za serikali ili kufatilia viongozi wa ngazi zote si madiwani na masheha peke yao kwani wapo baadhi ya viongozi wa ngazi za juu pia wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
chanzo:zanzibar24.
Comments